Rais Samia, Askofu Shoo walivyoing’arisha miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC

Muktasari:

  • Ni miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyoanzishwa mwaka 1971 na Hayati Askofu Stephano Moshi aliyekuwa na maono ya kuanzisha hospitali hiyo ili itoe huduma za tiba, mafunzo na kufanya utafiti mbalimbali wa magonjwa ya binadamu.

Moshi. Ni miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyoanzishwa mwaka 1971 na Hayati Askofu Stephano Moshi aliyekuwa na maono ya kuanzisha hospitali hiyo ili itoe huduma za tiba, mafunzo na kufanya utafiti mbalimbali wa magonjwa ya binadamu.

Tangu ilipoanzishwa mwaka 1971 hadi mwaka 1992, hospitali ya KCMC ilikuwa ikiendeshwa na Serikali, hata hivyo baadaye ilirudishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambao ndiyo wamiliki wa hospitali hiyo kupitia Shirika la Msamaria Mwema (GSF).

Serikali ilirejesha hospitali hiyo mikononi mwa uendeshaji wa kanisa hilo kwa makubaliano maalum kuwa kanisa litasimamia na kuendeleza miundombinu ya hospitali na Serikali italipa mishahara ya wafanyakazi wote.

Hivi sasa maono ya Askofu Stephano Moshi katika hospitali ya KCMC yanaendelea kuonekana kwani hospitali inatoa huduma za tiba, mafunzo na tafiti kwa Watanzania wote, bila kubagua kabila, rangi, imani au itikadi ya chama, na imekuwa ni baraka kwa wananchi wa kanda ya Kaskazini na hata nje ya mipaka.

Akizungumza katika kumbukizi ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC Kanda ya Kaskazini, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Msamaria mwema la Tanzania (GSF), ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini, na mkuu wa kanisa hilo Tanzania, Askofu Dk Fredrick Shoo alisema, “Napenda kuzipongeza awamu zote za Serikali kwa kuendelea kushirikiana na kanisa katika kusimamia hospitali hii na katika kutoa huduma za afya na kwa kipindi chote cha miaka 50 ya hospitali hii, Serikali imekuwa ikilipa mishahara ya watumishi, na kuchangia fedha za matumizi ya kawaida.”

Dk Shoo alieleza pia, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya hospitali hiyo, bado zipo changamoto mbalimbali. Changamoto hizo ni upungufu wa watumishi wa kada zote unaofikia 758, kutoidhinishwa kwa muundo wa utumishi (scheme of service) wa KCMC na kutotengewa fedha kwa kipande cha barabara chenye urefu wa mita 850.

“Kutokana na upungufu wa watumishi kwa ngazi zote, hospitali inalazimika kutumia kiasi kikubwa cha mapato ya ndani kujaribu kuziba pengo hilo, jambo ambalo linafifisha mipango yetu ya kuendelea kuboresha, kukarabati na kuweka miundombinu mipya,” alisema Dk Shoo.

Alisema, kutoidhinishwa kwa muundo wa utumishi KCMC kumesababisha watumishi kulipwa mishahara midogo ukilinganisha na hospitali nyingine za rufaa za kanda na kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyehudhuria kumbukizi hizo aingilie kati.

Alisema, “Ili kutatua changamoto hii, tunaomba hospitali yetu ipitishiwe muundo wake wa utumishi, kama zilivyopitiwa hospitali nyingine, tumeliomba hili kwa muda mrefu, lakini tunaambiwa tusubiri na wakati mwingine tunaambiwa haiwezekani, tunakuomba Rais katika hili utusaidie.”

Dk Shoo alitaja changamoto nyingine ni ubovu wa kipande cha mita 850 za barabara, ambayo inaingia Hospitali ya KCMC kupitia barabara ya Stephano Moshi ambacho wameomba kitengenezwe kwa muda mrefu na haijatengewa fedha hata kwenye bajeti ya mwaka huu.

Matarajio na malengo ya hospitali ya KCMC

Dk Shoo anasema hivi karibuni wanatarajia kuanza ujenzi wa kitengo cha moyo, ambapo kukamilika kwake, kutakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine.

Anasema ujenzi kitengo hicho cha moyo, utagharimu Sh16 bilioni, gharama ambazo zitafadhiliwa na GSF, pamoja na wafadhili kutoka Marekani, Uholanzi, Misri na kiasi kingine wanatarajia Watanzania watachangia ili kukamilisha mradi huo mkubwa, ndani ya miaka minne ijayo.

“Mipango ya ujenzi wa kitengo hiki tayari imeanza na tayari pia kuna wataalamu wamepelekwa shule ili mara tu wamalizapo mafunzo yao, wakute ujenzi wa jengo na uwekaji wa vifaa tiba umekamilika, ni matarajio yangu, Serikali nayo pia, itachangia kufanikisha ujenzi wa kitengo hiki, ”alisema Dk Shoo.

Alisema mipango mingine ni kujenga maabara ya kisasa ya kimataifa yenye uwezo mkubwa wa kuchakata sampuli mbalimbali na kutoa majibu kwa haraka, ambapo kukamilika kwake kutachochea utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.

“Vile vile tunao mpango wa kukamilisha ujenzi wa vyumba vinane vya kisasa vya upasuaji, sambamba na kujenga kitengo kitakachojihusisha na huduma za upasuaji wa uti wa mgongo na ubongo, na ombi letu kwa Serikali ni kutupatia watumishi kwa wakati, mara miradi hii itakapokamilika na sisi tutaendelea kuwaelimisha wale ambao Mungu atatuwezesha,” alisema Dk Shoo.

Alisema,“Tumekuwa tukianzisha miradi mingi lakini ukifika muda wa kuanza kutoa huduma tunakosa watumishi husika, ambapo katika makubaliano yetu ni kuwa shirika litaajiri kwa kibali cha serikali, lakini nasikitika kukuarifu mheshimiwa Rais kuwa katika kipindi cha miaka minne sasa, Serikali haijatoa kibali cha ajira mpya kwa hospitali yetu.”

Rais Samia alivyoshusha neema

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya hospitali ya KCMC, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliupongeza uongozi wa hospitali kwa kuendelea kutoa huduma bora za matibabu na mafunzo kwa Watanzania wote bila ubaguzi na kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kisasa.

Rais Samia alisema Serikali kwa kushirikiana na kanisa wameendelea kuiboresha hospitali hiyo ambapo hapo awali ilikuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 350 kwa wakati na sasa idadi ya vitanda imeongezeka hadi kufikia 686.

Alipongeza bodi ya GSF na uongozi wa KCMC kwa kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kisasa inayotumia vifaa vya kisasa kama CT Scan, MRI na kusema ametaarifiwa mashine zote za vipimo kwa ujumla wake ni 33.

Alisema hospitali hiyo imeendelea kujiimarisha katika huduma za kibingwa na kung’aa nchini na kimataifa hasa katika huduma za tiba za ngozi, tiba za macho, mfumo wa mkojo na uzalishaji wa viungo bandia na kwamba ubobezi wao katika huduma hizo umewezesha uwepo wa utalii tiba nchini na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

“Hospitali hii ina hadhi ya kuwa super specialized (hospitali za kibingwa bobezi). Lengo la serikali ni kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi,”alisema Rais Samia na kuwapongeza pia kwa kuanzisha huduma za matibabu ya ugonjwa wa Saratani.

Akizungumzia uhaba wa watumishi, Rais Samia alisema anatambua suala hilo ni changamoto inayozikabili hospitali zote nchini na kueleza kuwa ili kuajiri, kunahitajika uchumi uwe imara kuwezesha hilo.

“Tunapopiga hesabu za uchumi kuna kitu kinaitwa wage bill kwa hiyo hatuwezi kuvuka wage bill kama Serikali haiwezi kuvuka kiwango cha ukuaji uchumi. Kila pale tunapopata upenyo uchumi unapokua tunafanya haraka haraka kuajiri,”alisema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais, ajira hizo zimekuwa zikilenga kwanza maeneo ambayo yanagusa maisha ya watu kama madaktari, wauguzi na walimu, lakini akashangaa KCMC kukaa miaka minne bila kupewa kibali cha ajira.

“Inasikitisha kuona kwa miaka minne nyuma, KCMC haikuwahi kupata watumishi. Niwahakikishie baba Askofu tutakapopata tu upenyo wa kuajijri tutahakikisha KCMC nayo inapata Fungu Lake, ”alisema Rais na kuongeza,“ Ingawa si kwa kiwango chote cha upungufu, lakini tutaangalia maeneo muhimu Muundo wa utumishi umelia hapa, nikuahidi tutakwenda kuuangalia kwa nini ulikwama na kama kuna vikwazo tuvifanyie kazi kwa pamoja tusonge mbele.”

“Ni muhimu kuwa na muundo utakaoziweka sawa hospitali zetu na kuhakikisha watumishi wote wanapata stahili zao jinsi wanavyostahiki kulingana na majukumu yao. Miundombinu bora inayofikika ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha wananchi wanafikia huduma muhumu za afya. Serikali imesikia kilio chenu cha kutaka kuweka lami mita 850,”alisema Rais Samia.

Alisema, “Mbele yangu hapa nina waziri wa Ujenzi lakini nina waziri wa Tamisemi. Wanyewe watajipanga nani anaweza kulichukua lakini nikuhakikishie tutalifanyia kazi. Inawezekana si mwaka huu lakini kipande kile tutakiweka lami,”alisisitiza.

Alisema jengo la mionzi kwa ajili ya matibabu ya saratani litakalogharimu Sh4 bilioni ambalo Serikali iliahidi kugharamia ujenzi wake kwa asilimia 100, tayari KCMC wameshapokea Sh1 bilioni na kiasi kama hicho kiko njiani.

“Niwahakikishie kuwa fedha zote Sh4 bilioni zitaletwa ili jengo hili likamilike, tutahakikisha ujenzi unamalizika ili huduma zianze kutoka kwa haraka. Na hapa kuna Naibu Waziri wa Afya, (Dk Godwin Mollel), nikuagize muangalie njia zote zinazowezekana, kukamilisha jengo hili,” alisema Rais Samia.

Alisema, “Niupongeze uongozi wa KCMC kwa uthubutu na kuweza kuanzisha huduma za matibabu na uchunguzi wa saratani pamoja na ujenzi wa wadi ya wagonjwa wa saratani. Kuanzishwa kwa huduma hii, kumepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Ocean Road na hata kupeleka wagonjwa nje ya nchi,”alisema Rais Samia.

Rais Samia aliipongeza KCMC kwa mpango wa kuanzisha kitengo cha tiba ya moyo na kueleza kuwa Serikali iko tayari kuunga mkono jitihada hizo, maana zitaondoa mzigo mzito unaobebwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo inatibu moyo.