Rais Samia ataimarisha zaidi demokrasia ya vyama vingi

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walipokutana Ikulu jijini Dar es Salaam, Machi 4, 2022 kuzungumzia namna ya kufanya siasa kwa masilahi ya Taifa. Picha na maktaba

Muktasari:

Jitihada na dhamira ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira mazuri ya kuendesha shughuli za kisiasa nchini ni dalili njema za kuimarisha demokrasia.

Jitihada na dhamira ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira mazuri ya kuendesha shughuli za kisiasa nchini ni dalili njema za kuimarisha demokrasia.

 Mwezi uliopita Tanzania imeadhimisha miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, uamuzi uliofanywa na Bunge Mei 7, 1992 na kuidhinishwa rasmi Julai Mosi, 1992.

Uamuzi huo ulikuwa wa kufanya marekebisho ya kufuta ibara zilizokipa Chama cha Mapinduzi (CCM) haki pekee za kuendesha siasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku vipengele vingine vikirekebishwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Tayari chaguzi sita zimefanyika tangu mwaka 1995 hadi 2020, huku CCM ikiendelea kuibuka na ushindi na vyama vya upinzani vikimaliza uchaguzi kwa kukosoa uendeshaji wake na tuhuma nyingine za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu.

Ikiwa imetimia miaka 30, bado lawama za kuminya demokrasia ya vyama vingi imeendelea kuwapo kwa polisi kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani, madai ya demokrasia kuminywa ndani ya Bunge na madai ya chama tawala kunufaika na rasilimali za Serikali, ikiwamo magari na maofisi.

Hata hivyo, wakati ikitimia miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, kwa mujibu wa Shirika la misaada la Marekani (USAID), Tanzania bado iko kwenye viwango vya juu katika masuala ya uwazi, uwajibikaji na haki za kijamii, huku suala la demokrasia likionekana kulegalega.

Kenya ambayo ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kama ilivyo Tanzania, yenyewe ilianza mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991.

Hata hivyo, Kenya kwa sasa iko mbele katika masuala ya demokrasia ya vyama vingi baada ya kubadilishwa Katiba na sasa vyama vinaweza kuungana kwenye uchaguzi na kuunda Serikali tofauti na ilivyo Tanzania.

Kwa mfano, nchini Kenya kumekuwa na miungano ya vyama kama CORD Coalition, Jubilee Coalition, National Rainbow Coalition, Amani Coalition, EAGLE Coalition, National Super Alliance (NASA) Coalition, Kenya Kwanza Alliance na Azimio la Umoja Coalition.

Pia, sheria imepitishwa kuruhusu vyama kuungana bila kupoteza utambulisho wao na kuunda Serikali kwa pamoja.


Matumaini kwa Tanzania

Matumaini ya Tanzania kuweza kuwa na demokrasia pana kwenye mfumo wa vyama vingi yameanza hasa katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni Aprili 22, 2021.

Rais Samia alieleza mwelekeo wa Serikali yake ndani ya Bunge kuhusu nia yake ya kutaka kukutana na kuzungumza na vyama vya upinzani.

Kwa kuthibitisha nia yake hiyo, Rais Samia alikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na walizungumza mambo kadhaa ya kujenga siasa zenye ushindani wa hoja na uwanja sawa wa siasa.

“Kitu kikubwa tulichojadiliana ni kuwa, Tanzania ni yetu sote na tunapaswa kufanya kazi pamoja, kuijenga, lakini hili linawezekana tu iwapo tutajenga uaminifu na kudai haki, pamoja na kuheshimiana. Hii itatusaidia kupata nafasi ya kuijenga nchi yetu,” ilikuwa ni kauli ya Rais Samia baada ya mazungumzo yake na Mbowe.

Huku Mbowe akisema: “Tumekubaliana kuwa, njia nzuri ya kuwa na maridhiano ni wakati kuna haki. Tumepitia madhila mengi, hakuna haja ya kuyarudisha mara kwa mara, badala yake tunapaswa kusonga mbele na kuwa na siasa safi na kuiunga mkono Serikali, na tunatumai kuwa itatuunga mkono kwenye shughuli zetu ili kila mtu afurahi.

Mbali na kukutana na Mbowe, Rais Samia akiwa na viongozi wa CCM na Serikali walikutana na viongozi wa Chadema, wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya chama hicho.

Miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni maridhiano katika uwanja wa siasa, ikiwamo hoja ya Katiba mpya na kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Pia, Rais Samia alikutana na viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo katika mwendelezo wake wa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kama alivyoahidi kwenye hotuba yake bungeni.

Desemba mwaka jana, Rais Samia alihutubia mkutano wa wadau wa kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini na baada ya mkutano huo aliunda kikosi cha kujadili mapendekezo ya wadau wa siasa yatakayofanyiwa kazi na Serikali.

Kikosi kazi hicho kilifanya kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Rais Samia, aliyetoa kauli iliyoonyesha matamanio yake kuona Tanzania inaendelea kuwa moja na salama bila kuwa na kundi litakalohisi kuachwa nyuma katika safari ya kufurahia demokrasia ya kweli.

Pia, Rais Samia aliwataka wajumbe wa kikosi hicho kwenda kunoa bongo zaidi ili hatimaye kuwasilisha ripoti itakayojibu njia bora za kuzitafutia majawabu ya changamoto ambazo nyingine ametaka zitafutiwa ufumbuzi wake wa haraka hata kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.


Msimamo wa CCM

Kubadilika kwa msimamo wa Chama tawala kuhusu hoja ya katiba mpya ni ishara nyingine kwamba katika siku zijazo demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania itaimarika zaidi.

CCM kupitia kwa Shaka Hamdu Shaka ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, aliutangazia umma wa Watanzania kwamba wamekubali mchakato wa Katiba mpya ufufuliwe kwa masilahi ya taifa.

Kwa CCM kukubali hoja ni dalili kwamba demokrasia ya vyama vingi kwa Tanzania katika miaka ijayo itabadilika na kuwa imara zaidi.


Maoni ya mdau

Akizungumzia demokrasia ya vyama vingi nchini, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema ana matumaini kwa kuwa safari ni hatua.

Anasema Tanzania ilikotoka kumekuwa na changamoto nyingi za kupanda na kushuka, lakini kwa miaka 30 hali ni nzuri kwa kuwa baadhi ya vyama (Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF) vilivyoanza tangu mwaka 1992 bado vipo.

Dk Loisulie alisema kinachohitajika ni maridhiano kwa wanasiasa ili kuwe na uhuru wa kutoa maoni na wa kufanya siasa.

Alisema Rais Samia ameonyesha njia ya kuleta demokrasia ya kweli nchini kwa kuweka maridhiano ya kisiasa.

“Kwa vyama vya siasa kinachohitajika ni nidhamu, kwani uhuru ukipitiliza hata vyama vyenyewe vinaweza kufa,” alisema.