Rais Samia ataja fursa za ajira akipigia chapuo Vyuo vya Amali

Rais Samia Suluhu Hassan akiupungia mkono umati wa wananchi waliojitokeza kumpokea alipowasili kuweka jiwe la msingi katika Chuo cha Amali mjini Igunga.

Muktasari:

Rais Samia yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora anakotarajiwa kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo

Tabora. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Serikali wa kujenga Vyuo vya Amali katika maeneo mbalimbali nchini unalenga kutoa fursa kwa wanafunzi mafunzo kwa vitendo utakaowapa ujuzi wa kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.

Akihutubia wananchi mjini Igunga leo Octoba 17, 2023, Rais Samia amesema vyuo hivyo pia vitatoa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

‘’Vijana wetu wanakosa sifa na nafasi zao za ajira katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali inachukuliwa na wageni kwa sababu hawana ujuzi…vyuo hivi tunavyojenga katika halmashauri mbalimbali nchini vitatoa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika,’’ amesema Rais Samia

Mkuu huyo wan chi amesema vyuo hivyo pia vitatumika kuwapa vijana ujuzi utakaofanikisha lengo la kuwajengea kesho bora kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyobora (BBT) inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Amesema ili kufikia lengo la kunufaisha vijana wa maeneo yote nchini, ujenzi wa vyuo vya amali utazingatia ujuzi kulingana na eneo husika.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo ametumia mkutano huo kuwasihi wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika vyuo hivyo ili wapate ujuzi na maarifa utakaowawezesha kumuda maisha.

Rais Samia yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora anakotarajiwa kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.