Rais Samia ataka mageuzi sekta ya fedha yamguse mwananchi wa chini
Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu, Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za fedha kutoa mikopo kwa kuzingatia uaminifu wa wateja badala ya dhamana za mali pekee, huku akisisitiza mageuzi ya uchumi yawaguse wananchi moja kwa moja.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mageuzi yanayofanyika katika sekta ya fedha yanapaswa kuakisi maisha halisi ya wananchi badala ya kubaki kwenye takwimu huku yakitofautiana na hali halisi ya maisha ya watu kule chini.
Pia, amezitaka taasisi za fedha nchini kuwa wabunifu katika kutafuta njia zitakazowawezesha kutoa mikopo kwa wananchi bila kuhitaji dhamana zilizozoeleka kama vile nyumba, gari au kiwanja, bali watumie uaminifu wao katika biashara wanazozifanya.
Rais Samia amebainisha hayo leo Juni 12, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 1966, ikiwa na jukumu la udhibiti wa sekta ya fedha.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri, magavana na naibu magavana wastaafu, wafanyakazi wa BoT, wafanyakazi wa Wizara ya Fedha, wawakilishi wa mashirika ya fedha pamoja na mabalozi.
Akizungumza wakati wa hotuba yake, Rais Samia amesema ni muhimu kwa BoT kuimarisha uwezo wake wa kung’amua mapema mwelekeo wa taifa kiuchumi katika muktadha wa mabadiliko ya kidunia.
Mkuu huyo wa nchi amesema kila mtu ni mshahidi wa masuala yanayoendelea duniani, ikiwemo misukosuko ya kisiasa na namna inavyoathiri uchumi wa dunia kwa ujumla.
Amesema misukosuko hiyo inaathiri upatikanaji wa bidhaa, uhimilivu wa mifumo ya fedha pamoja na thamani ya sarafu ndani ya muda mfupi. Amesema changamoto hiyo imejidhihirisha kwenye mafuta ambapo kwa sasa yamepanda bei na kusababisha kupanda kwa bei za bidhaa nyingine.
Ameongeza kuwa hayo yanakumbusha kuwa ushindani wa kimataifa unaotukabili sasa si rasilimali na uzalishaji peke yake, bali uwezo wa nchi kutabiri na kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa na kiuchumi ya dunia.
Rais Samia amesema kaulimbiu hiyo imebeba kile kinachoendelea duniani kote, kwa kuwa mabadiliko hayo yataleta mageuzi ya kiuchumi, hivyo Benki Kuu inapaswa kuwa wabunifu ili kustahimili yale yanayotokea.
“Mageuzi tunayoyazungumza ni muhimu lakini kama hayabadili maisha ya wananchi yatasalia kuwa takwimu katika ripoti zetu. Takwimu zitasema kama tunavyoona upande mwingine, uchumi unapanda, GDP ni kubwa, uchumi wa nchi ni mkubwa lakini ukifika kwa watu hali za watu siyo nzuri,” amesema.
Amesisitiza kwamba wasiposimamia vema, mabadiliko hayo yatabaki kuwa takwimu na ni vema kutafsiri ukuaji wa uchumi ili uende ukakue mpaka kwa mtu wa kawaida kule chini.
Amesema ustahimilivu ni muhimu lakini bila kujenga uwezo wa ndani kisera na kifedha, unaweza kuwa na uwezo wa kuvumilia matatizo badala ya kuwa na uwezo wa kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili.
“Mafanikio katika mifumo ya fedha hayana budi kwenda na mafanikio ya mwananchi mmoja. Kipimo chetu kisibaki kuwa ni wananchi wangapi wamefikiwa na huduma ya fedha, bali tujipime ni kwa kiasi gani huduma za fedha zinakuza mitaji na biashara ndogondogo na kuweza kuchangia kuwafanya wale wa biashara ndogondogo kuchangia katika uchumi wa nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Pamoja na hayo tujiulize pia ni wangapi wameongeza kipato, ni biashara gani zimepanuka, ni wakulima wangapi wamepata mitaji kwa wakati, ni vijana wangapi wamegeuza mawazo yao kuwa kampuni na familia ngapi zimejenga akiba inayoweza kuwanusuru wakati wa changamoto.”
Rais Samia amesema maswali hayo yanafikirisha kuhusu nafasi ya sekta binafsi ambayo ndiyo nguzo kuu ya uzalishaji, uwekezaji na ajira.
Amesema kadiri sekta binafsi inavyopata mitaji kwa gharama nafuu na kwa masharti yanayoendana na uhalisia wa biashara, ndivyo fursa zinavyoongezeka, biashara zinavyopanuka na uzalishaji unavyokua au kuongezeka.
Rais Samia amesisitiza haja ya kumsikiliza mwananchi anapolalamikia riba ya mikopo kuwa kubwa, asijibiwe kwa takwimu za kiuchumi peke yake, bali wafuatilie wanalalamikia kitu gani na kurekebisha.
“Kwa mtu wa kawaida, gharama ya mkopo inajumuisha riba, ada, bima, masharti, dhamana na muda unaotumia kuupata mkopo wenyewe. Hiyo ndiyo gharama kubwa ya mikopo kwa watu wetu.
“Ili kuisaidia sekta isiyo rasmi, tuwe na mipango ya kuhakikisha taasisi zote za kifedha zinaimarisha uwazi kuhusu gharama za mikopo inayotolewa kwa wananchi,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa mwananchi apewe taarifa sahihi na kwa lugha nyepesi, kiasi atakacholipa, kwa kipindi gani na kwa gharama gani kabla hajafanya uamuzi wa kuchukua mkopo husika.
“Tuendelee kuimarisha mifumo ya riba inayotumia mifumo ya Benki Kuu ili uende kumgusa moja kwa moja mkulima, mjasiriamali na mzalishaji mdogo,” amesema Rais Samia akiielekeza Benki Kuu.
Rai kwa taasisi za fedha
Rais Samia amezitaka taasisi za fedha kuongeza ushindani katika utoaji wa mikopo na kuacha kutegemea aina za dhamana ambazo wananchi wengi hawana, kama vile hati za nyumba, maeneo wala magari, lakini wana biashara, historia nzuri ya mauzo, kumbukumbu za miamala zinazoaminika na uwezo wa kurejesha mikopo.
“Hawa wafikirieni, tafuteni njia mnazoweza kuwaingiza wakaaminika, wakapata mikopo. Tusimnyime mtu mkopo kwa sababu hana mali tuliyozoea kuitambua wakati ana historia inayoonyesha wazi anaaminika. Uaminifu ni asset kubwa kuliko hata mali inayoonekana,” amesema Rais Samia.
Amezitaka taasisi za fedha nchini kuwa wabunifu katika kutafuta mbinu rahisi za kuhakikisha mikopo inatolewa na kurejeshwa bila kuwepo kwa vikwazo visivyo vya lazima kwa wajasiriamali wadogo na biashara za kati.
“Tafakarini namna ya kujenga mfumo ambao Mtanzania anaweza kubeba historia yake ya uaminifu wa kifedha popote anapokwenda. Mama lishe asiye na nyumba lakini mwenye historia ya miaka mitano ya biashara na malipo, anapaswa kuwa na njia rahisi ya kuthibitisha kuwa anastahili mkopo.
“Hili niwaachie kama changamoto, mkalifanyie kazi, Benki Kuu na taasisi zote za fedha ili kufungua milango kwa mamilioni ya wananchi walio nje ya mfumo wa mikopo rasmi,” amesisitiza Rais Samia katika hafla hiyo.
Mageuzi ya uchumi
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema katika safari hiyo ya miaka 60 wanatambua juhudi kubwa zilizofanywa na viongozi wa Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kwa mchango wao katika kuijenga Benki Kuu.
Amesema maadhimisho hayo yanawapa nafasi ya kutathmini safari ya ukuaji wa uchumi, uhimilivu na mchango wa Benki Kuu katika kujenga uchumi jumuishi, sarafu imara na ujumuishi wa kifedha.
Tangu mwaka 1966, BoT imepitia mageuzi tofauti ya kisiasa na kiuchumi ikiwamo mabadiliko ya kisera na mifumo ya kifedha. Amesema sekta ndogo ya benki ilikuwa na mchango mdogo katika uchumi, takribani asilimia 20 katika sekta ya fedha, hadi kufikia mwaka 1991.
“Uchumi ulikuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 20 na ukuaji wa uchumi uliokuwa chini ya asilimia tano,” amesema Tutuba wakati wa hotuba yake.
Katika miaka mitatu iliyopita, Tutuba amesema kiwango cha mfumuko wa bei kilikuwa kwa wastani wa asilimia 3.5, akiyataja kuwa ni mafanikio ukilinganisha na mwaka 1994 ambapo kiwango cha mfumuko wa bei kilikuwa wastani wa asilimia 35.3.
Akiba ya dhahabu
Tutuba amebainisha kwamba hadi kufikia Juni 10, 2026, BOT imehifadhi akiba ya dhahabu ya tani 27.5 yenye thamani inayokadiriwa kufikia Sh10 trilioni.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Benki Kuu kuimarisha akiba ya taifa na kuongeza uthabiti wa uchumi wa nchi kupitia uwekezaji katika madini ya dhahabu kama mali salama ya kifedha.
“Mpaka kufikia Juni 10, 2026, Benki Kuu ina dhahabu tani 27.5 zenye thamani ya takribani Sh10 trilioni,” amesema Tutuba.
Aidha, BoT imekuwa ikiweka wazi mkakati wake wa kuongeza akiba ya dhahabu kwa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa ndani kupitia utaratibu rasmi wa kibenki. Hatua hiyo imekuwa ikielezwa kuwa na lengo la kuongeza akiba ya taifa, kupunguza utegemezi wa fedha za kigeni katika dhahabu, na kuimarisha uthabiti wa shilingi ya Tanzania.
Siri ya BoT
Awali, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema miaka ya 1960 hadi 1965 nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru na wakati huo kulikuwa na Bodi ya Sarafu za Afrika Mashariki, ikiwa na wanachama wanne.
Amesema kazi ya bodi hiyo ilikuwa ni kutoa sarafu iliyojulikana kama Shilingi ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, amesema hifadhi ya sarafu hiyo ilikuwa Benki Kuu ya Uingereza ambayo ndiyo ilizitawala nchi hizo za Afrika Mashariki wakati huo.
“Kwa maana hiyo, tulikuwa na uhuru wa kisiasa, lakini hatukuwa huru kiuchumi. BoT ni ishara ya uhuru wetu,” amesema Balozi Omar ambaye amefanya kazi katika sekta ya fedha kwa muda mrefu kabla ya kuteuliwa kuwa waziri.