BoT yataka pengo la kijinsia huduma za kifedha kufutwa
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Sauda Kassim Msemo.
Muktasari:
- Wanawake bado nyuma katika upatikanaji wa huduma, taasisi zahimizwa kutumia data kubuni suluhu
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema bado kuna pengo kubwa la kijinsia katika upatikanaji wa huduma za kifedha nchini, ikisisitiza umuhimu wa hatua za makusudi kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika mfumo rasmi wa kifedha.
Akifungua warsha ya siku mbili jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Juni, 8, 2026, Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema kuziba pengo hilo ni moja ya vipaumbele vya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Ujumuishi wa Kifedha.
Amesema takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha wanawake bado wapo nyuma katika matumizi ya huduma za kifedha ikilinganishwa na wanaume, jambo linalopunguza fursa zao za kukuza biashara na kujikwamua kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 18 ya wanawake wanapata huduma za kifedha dhidi ya asilimia 26 ya wanaume.
“Iwapo tutafikia kiwango cha wanaume cha mwaka 2023 kwa upande wa wanawake, tutakuwa tumepiga hatua kubwa. Hata hivyo, lengo letu ni kufikia asilimia 85 ya ujumuishi wa kifedha ifikapo mwaka 2028,” amesema Msemo.
Amebainisha kuwa BoT itaendelea kutoa miongozo ya kisera, kanuni na uratibu unaohitajika ili kuweka mazingira yatakayowezesha taasisi za fedha kuwafikia wanawake wengi zaidi.
Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanategemea ushirikiano kati ya taasisi za fedha, wadau wa maendeleo na mamlaka za usimamizi wa sekta hiyo.
Msemo pia amezitaka taasisi zinazoshiriki warsha hiyo kutumia maarifa yatakayopatikana kubuni bidhaa na huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji halisi ya wanawake katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema matumizi ya takwimu zilizochanganuliwa kwa kuzingatia jinsia yatasaidia taasisi za fedha kuelewa changamoto zinazowakabili wanawake na hivyo kubuni suluhu zinazoongeza ushiriki wao katika mfumo rasmi wa kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Benki Tanzania (TBA), Tuse Joune amesema uwekezaji katika ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake ni mkakati muhimu unaochochea maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema wanawake wanapopewa fursa za kifedha huongeza tija katika biashara zao, familia na jamii zinazowazunguka. Amefafanua kuwa mara nyingi wanawake huwekeza mapato yao katika elimu, afya na ustawi wa familia, hatua inayochangia kujenga jamii imara.
“Wanawake wana athari kubwa chanya katika maendeleo ya jamii. Kuwajengea uwezo ni sehemu ya kuimarisha ustawi wa Taifa lote,” amesema.
Tuse amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa We-Finance Code nchini mwaka jana, sekta ya benki imeanza kufanya maboresho yanayolenga kuelewa mahitaji ya wanawake na kuboresha huduma zinazotolewa kwao.
Naye mwakilishi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), Milena Stefanova, amesema We-Finance Code ni mpango wa kimataifa unaolenga kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake wajasiriamali kupata huduma za kifedha na mitaji ya kukuza biashara zao.
Amesema mwongozo huo, ulizinduliwa mwaka 2023, unatekelezwa katika nchi 33 duniani kufikia Juni 2026, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika katika utekelezaji wake.
Stefanova amesema wanawake nchini wanaunda sehemu kubwa ya wamiliki wa biashara ndogo na za kati, lakini bado wengi hawajafikiwa kikamilifu na huduma rasmi za kifedha.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa We-Finance Code yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wasimamizi wa sekta ya fedha, benki za biashara na taasisi za maendeleo ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kiuchumi na kifedha.