Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BOT yajivunia miaka 60 ya kulinda uchumi, kuimarisha sera za fedha

Wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mbeya pamoja na wadau wa taasisi za kifedha wakiwa katika maandamano kuelekea Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya BoT tangu kuanzishwa kwake, ambapo kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Juni 12 mwaka huu. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imesema katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kusimamia utulivu wa uchumi, kuimarisha sera za fedha na kuhakikisha upatikanaji wa sarafu nchini, huku ikiahidi kuendelea kutoa elimu na huduma kwa wananchi.

Mbeya. Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Tawi la Mbeya imesema imefanikiwa kutekeleza jukumu lake la kusimamia sera za fedha, kudumisha utulivu wa uchumi kwa kuhakikisha upatikanaji wa sarafu nchini katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi, Juni 6, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Tawi la Mbeya James Machemba, wakati wa maadhimisho ya miaka 60 yaliyo fanyika katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Awali , maadhimisho hayo yalianza maandamano sambamba na michezo mbalimbali katika Viwanya vya Kumbukumbu ya Sokoine iliyo husisha wafanyakazi na wadau wa taasisi za kifedha.

Kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kinatarajiwa kufanyika Juni 12, 2026 jijini Dar es Salaam.

Machemba amesema maadhimisho hayo yanalenga kuonyesha mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa na kuhamasisha wananchi kuelewa majukumu ya benki hiyo.

"Tunatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), katika kipindi hiki tumeendelea kusimamia sera za fedha, kuhakikisha upatikanaji wa sarafu na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi," amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akisalimiana na wafanyakazi na wadau walioshiriki michezo ya maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Amesema BOT imewashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya fedha, ikiwemo benki za biashara, katika shughuli hizo ili kuimarisha ushirikiano na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za kifedha.

Aidha, amesema kwa matawi ya mikoani maadhimisho hayo yameambatana na utoaji wa misaada kwa makundi yenye uhitaji maalumu kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.

"Kwa miaka 60 tunajivunia utendaji wa kitaalamu na usimamizi madhubuti wa sera za fedha ambao umewezesha uchumi wa Tanzania kuendelea kukua licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza duniani," amesema.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Idara ya Fedha, Beatrice Lyimo amesema michezo imepewa kipaumbele katika maadhimisho hayo kwa kuwa inachangia afya njema na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi na wadau.

"Wafanyakazi wengi hutumia muda mwingi wakiwa ofisini, hivyo tumeona ni muhimu kutumia maadhimisho haya kujenga afya na kuimarisha ushirikiano kupitia michezo," amesema.

Naye Kaimu Meneja wa Fedha na Utawala wa BOT Tawi la Mbeya, Ladislaus Kiwanga amesema ushiriki wa wadau mbalimbali unalenga kuwapa wananchi fursa ya kufahamu zaidi majukumu la benki hiyo na mchango wake katika ustawi wa uchumi wa taifa.

Mkazi wa Jakalanda, Tausi Azory, amesema maadhimisho hayo yameonyesha ushirikiano mkubwa uliopo kati ya taasisi za kifedha na wananchi, akiiomba BOT kuongeza utoaji wa elimu ya fedha na uchumi hususan maeneo ya vijijini.

"Wananchi wengi bado wanahitaji elimu kuhusu hali ya uchumi, matumizi sahihi ya fedha na umuhimu wa taasisi za kifedha. Maadhimisho kama haya yafike hadi vijijini," amesema.