Gavana: Wahasibu, wakaguzi wa hesabu ni nguzo ya Dira 2050
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, akizungumza jijini Arusha leo Jumatatu, Mei 25, 2026, katika semina ya pamoja ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na BoT iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha mfumo wa fedha endelevu kwa kutumia teknolojia.
Muktasari:
- Licha ya changamoto za uchumi duniani, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi huku sekta ya fedha ikiendelea kuwa himilivu
Arusha. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema wahasibu, wakaguzi wa hesabu na washauri elekezi wa masuala ya kifedha wana nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia usimamizi bora wa fedha, uwajibikaji na matumizi salama ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya fedha.
Amesema licha ya changamoto za uchumi duniani, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi huku sekta ya fedha ikiendelea kuwa himilivu.
Tutuba amesema hayo leo Jumatatu Mei 25, 2026 jijini Arusha wakati akifungua semina ya pamoja kati ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na BoT iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha mfumo wa fedha endelevu kwa kutumia teknolojia pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora katika sekta ya fedha na uhasibu.
Amesema wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wana wajibu mkubwa katika kusimamia masuala ya mazingira, kijamii na utawala bora (ESG), ambayo ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu ya uchumi wa Taifa.
“Kongamano hili limejadili namna ya kuimarisha usimamizi wa fedha kwa kuwashirikisha wahasibu, wakaguzi wa hesabu pamoja na washauri elekezi wa masuala ya fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa imara zaidi,” amesema Tutuba.
Amesisitiza umuhimu wa wataalamu hao kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuzingatia miiko ya taaluma pamoja na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika maeneo yao ya kazi.
“Dunia inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa wataalamu kuendelea kujifunza na kuendana na mabadiliko hayo badala ya kufanya kazi kwa mazoea,” amesema.
Kwa mujibu wa Tutuba, Tanzania imeendelea kuwa na ukuaji mzuri wa uchumi licha ya changamoto mbalimbali za kimataifa.
“Mwaka jana uchumi ulikua kwa asilimia sita na mfumuko wa bei uliendelea kubaki ndani ya wigo wa muda wa kati kwa asilimia 3.3,” amesema.
Hata hivyo, amesema bado kuna haja ya kuendelea kusimamia kwa karibu vihatarishi vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri sekta ya fedha.
Amesema wahasibu, wakaguzi wa hesabu na washauri wa masuala ya fedha ni wadau muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani ifikapo mwaka 2050 pamoja na pato la wastani wa Dola 7,000 kwa mwananchi mmoja mmoja.
Tutuba amewataka wataalamu hao kuhakikisha taasisi wanazozihudumia zinaendeshwa kwa uwazi na ufanisi ili kuzuia mianya ya uvujaji wa fedha.
Aidha, amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika miamala ya kifedha badala ya kutegemea fedha taslimu ambazo zina vihatarishi mbalimbali.
“Hakuna haja ya kubeba fedha taslimu kwa sababu kuna hatari nyingi ikiwemo kupotea au kuibiwa. Teknolojia za kidijitali zinawezesha miamala kufanyika kwa urahisi na usalama zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuongeza ubunifu na kushirikiana na wadau wengine katika matumizi ya teknolojia ili kuongeza mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa National Board of Accountants and Auditors, Siasa Mzenzi amesema semina hiyo imejikita katika kujadili uendelevu wa sekta ya fedha pamoja na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa fedha.
Amesema kongamano hilo limefanyika chini ya makubaliano ya ushirikiano kati ya NBAA na BoT kwa lengo la kuunganisha utaalamu wa taasisi hizo katika kuimarisha sekta ya fedha nchini.
“BoT ni wataalamu wa masuala ya fedha na sisi ni wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu, hivyo tumeona umuhimu wa kushirikiana ili kuhakikisha masuala yote ya fedha yanafanyika kwa kuzingatia taratibu na misingi ya kitaalamu,” amesema Profesa Mzenzi.
Amesema mjadala mkubwa katika kongamano hilo umejikita katika masuala ya mazingira, kijamii, utawala bora pamoja na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa endelevu na salama zaidi.
Kwa mujibu wa Profesa Mzenzi, matumizi ya teknolojia na bunifu mbalimbali yataendelea kusaidia kuhifadhi fedha kwa usalama, kuongeza uwazi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.