Prime
Wataalamu waeleza hatari ya kutumia vyeti kama dhamana ya mikopo
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Serikali tayari imeweka bayana mpango wa kuandaa Sheria ya Dhamana kwa Mali zinazohamishika itakayoruhusu vyeti vya elimu na mali nyingine zisizoshikika kutumika kama dhamana ya mikopo.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kukamilisha maandalizi ya sheria itakayoruhusu matumizi ya mali zinazohamishika ikiwamo vyeti vya taaluma kama dhamana ya mikopo, wataalamu wa uchumi na sheria wamesema mpango huo unahitaji mfumo imara wa udhibiti, usajili na tathmini ya dhamana hizo mpya.
Wakizungumza na Mwananchi leo Mei 21, 2026 wataalamu hao wamesema licha ya ubunifu wa mpango huo, Serikali italazimika kuweka mifumo madhubuti ya usajili, tathmini na udhibiti wa dhamana hizo ili kuepusha hatari kwa taasisi za kifedha.
Serikali tayari imeweka bayana mpango wa kuandaa Sheria ya Dhamana kwa Mali zinazohamishika itakayoruhusu vyeti vya elimu na mali nyingine zisizoshikika kutumika kama dhamana ya mikopo.
Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo na kubadili mfumo wa upatikanaji wa mikopo nchini.
Aprili 9, 2026 akiwa bungeni Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba alisema mpango wa kutaka vijana watumie vyeti kama dhamana uko katika hatua nzuri na wakati ukifika watapeleka bungeni ili kuitungia sheria ya dhamana inayohamishika.
Alisema hali ilivyo sasa, wasomi wengi wamelundikana bila kazi na kwa baadhi ya maeneo wamekuwa ni mzigo kwa wastaafu waliowasomesha.
Hoja hiyo imeibuka tena bungeni leo Mei 21, 2026 wabunge wa viti maalumu Neema Majule na Esther Matiko walitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wahitimu kutumia vyeti vyao kupata mikopo ya kuanzisha miradi ya maendeleo.
Akijibu kuhusu hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa Sheria ya Dhamana kwa Mali Zinazohamishika, inayolenga kutambua rasmi mali hizo katika mfumo wa utoaji wa mikopo.
Amesema chini ya sheria hiyo, mali zinazohamishika zitakuwa zinasajiliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuimarisha usimamizi, uwazi na ufuatiliaji wa dhamana hizo.
“Miongoni mwa mali zinazopendekezwa kufanyiwa tathmini ni vyeti vya taaluma vya wahitimu wa vyuo, kwa lengo la kuchunguza uwezekano wa kuvifanya vitumike kama dhamana katika upatikanaji wa mikopo,” amesema Lwesutula.
Akizungumza na Mwananchi, wakili na mtaalamu wa sheria za fedha ambaye hakutaka jina lake linukuliwe gazetini amesema kimsingi hakuna kizuizi cha moja kwa moja cha kisheria kinachokataza Serikali kutambua mali zisizoshikika kama dhamana, mradi tu sheria mpya itazingatia uwazi na uthabiti wa usajili wa mali hizo.
Amesema changamoto kubwa si uhalali wa kisheria bali ni namna ya kuthibitisha thamani ya chombo hicho kama dhamana.
“Sheria ya sasa, ikiwamo Sheria ya Ardhi Sura ya 113, imejikita zaidi kwenye mali zisizohamishika kama ardhi na majengo. Hivyo kuingiza vyeti kama dhamana kunahitaji mfumo mpya wa kisheria unaotambua ‘intangible assets’ na kuzisajili rasmi,” amesema wakili huyo.
Amesema mpango wa Serikali wa kuhusisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika usajili wa mali hizo unaweza kuwa msingi muhimu wa kuanzisha mfumo huo.
Hata hivyo, wataalamu wengine wanaeleza wasiwasi wao kuhusu hatari ya kifedha endapo vyeti vitatumika bila mfumo madhubuti wa tathmini ya hatari.
Akizungumzia hilo mwanasheria, Damaris Akaro amesema tofauti na ardhi au nyumba, vyeti vya elimu havina thamani ya moja kwa moja ya soko, jambo linaloweza kufanya taasisi za fedha kukosa usalama endapo mkopaji atashindwa kurejesha mkopo.
“Kisheria unaweza kuandika dhamana, lakini changamoto ni namna ya kuzipima thamani yake endapo mkopo hautalipwa. Je, cheti kitauzwa? Kitazuiwa vipi? Hapo ndipo mgongano wa kisheria na kiutendaji unapokuja,” amesema Damaris.
Hoja hiyo imeelezwa pia na Profesa wa Uchumi, Abel Kinyondo ambaye amesisitiza kuwa kinachohitajika ni kuangaliwa upya kwa dhamana ambazo hazitakuwa ngumu kwa wakopaji na hazitakuwa na hatari kwa benki.
“Huu mjadala ni matokeo ya Serikali kuona dhamana zilizopo kwenye mfumo wa benki sasa ni ngumu kubebwa na watu wengi, hivyo imekuja na wazo hili zuri ili kulisaidia kundi kubwa, lakini je usalama wake ukoje? Thamani ya vyeti inaweza kuendana na mkopo uliotolewa.
“Kwa kawaida dhamana ni mali isiyohamishika ambayo inaendana na thamani ya mkopo, hivyo mtu akishindwa kulipa deni mali hiyo inaweza kuuzwa na fedha zikatumika kulipa mkopo wake, sasa mtu akichukua mkopo kwa dhamana ya cheti halafu akashindwa kulipa utauza nini kufidia hilo deni,”amesema.
Profesa Kinyondo ameshauri Serikali kukaa chini na wadau katika sekta ya benki na kuangalia upya dhamana zinazoweza kuwekwa kwa ajili ya mikopo ili kuwezesha wananchi wa kawaida kumudu na zisizo na hatari kwa mabenki.
Kwa upande wake mchumi, Alfredy Urasa amesema mpango wa kutumia vyeti vya elimu kama dhamana ya mikopo unaweza kuwa na upungufu mkubwa wa kiuchumi na kibenki iwapo hautapitiwa kwa kina kabla ya utekelezaji.
Urasa amesema ingawa lengo la Serikali ni zuri la kupanua upatikanaji wa mikopo kwa vijana, mfumo wa benki unahitaji dhamana zinazoweza kupimika, kuuzwa na kurejesha thamani ya mkopo endapo mkopaji atashindwa kulipa, jambo ambalo vyeti vya elimu haviwezi kulitimiza kwa urahisi.
Amesema tatizo la msingi si upatikanaji wa dhamana pekee, bali ni usalama wa mfumo wa fedha na uwezo wa taasisi za kifedha kudhibiti hatari za mikopo.
“Benki haziwezi kufanya kazi kwa dhamana ambazo hazina soko la moja kwa moja. Cheti hakina thamani ya kibiashara inayoweza kuuzwa ili kurejesha mkopo. Hii inaweza kuongeza kiwango cha mikopo chechefu na kuhatarisha uthabiti wa sekta ya fedha,” amesema Urasa.
Ameongeza kuwa, hata kama Serikali itaweka mfumo wa usajili kupitia BoT, bado changamoto ya msingi itabaki kuwa namna ya kuthaminisha vyeti hivyo kwa viwango vinavyokubalika kimataifa katika masuala ya mikopo.
Mchumi huyo amesema badala ya kuingiza vyeti kama dhamana, Serikali inapaswa kuimarisha mifumo mbadala ya udhamini kama vile mifuko ya Serikali ya dhamana, inayoweza kushirikiana na benki kupunguza hatari kwa wakopeshaji huku ikiwasaidia vijana kupata mikopo.
“Suluhisho si kupanua aina ya dhamana bila mipaka, bali ni kuimarisha mifumo ya udhamini inayopunguza hatari kwa benki na wakati huo huo ikiwapa vijana nafasi ya kupata mitaji,” amesema.
Pia, amesisitiza kuwa, bila tahadhari hiyo, mpango huo unaweza kuongeza mzigo kwa benki na hatimaye kusababisha taasisi hizo kuwa na masharti magumu zaidi kwa wakopaji wote, jambo linaloweza kuathiri sekta nzima ya mikopo nchini.
Wakati hao wakieleza hivyo, mchumi Selestine Makaranga amesema mfumo huo ukiandaliwa vizuri, unaweza kuondoa utegemezi wa dhamana za jadi kama ardhi na kuwawezesha vijana kutumia rasilimali yao kuu ya elimu kama nyenzo ya kiuchumi.
“Faida kubwa ni kuongeza usawa wa fursa. Vijana wengi wana mawazo ya biashara lakini hawana mali. Kama elimu itatambuliwa kama dhamana, itaongeza ubunifu na ujasiriamali,” amesema Selestine.
Wakati akiuliza swali la nyongeza mbunge Matiko alihoji utayari wa Serikali kuweka mfumo maalumu utakaowawezesha wahitimu kutumia taaluma na vyeti vyao kama dhamana ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha ili waanzishe biashara na viwanda vidogo vidogo.
“Nataka kujua Serikali iko tayari sasa kuanzisha Graduate Credit Guarantee Scheme, itawezesha wahitimu hawa kutumia taaluma zao na vyeti vyao kama dhamana ili waweze kupata mitaji,” alihoji mbunge huyo bungeni.
Pendekezo hilo limekuja wakati tafiti mbalimbali zikionesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wahitimu wa vyuo nchini hukosa ajira rasmi, hali inayowaacha vijana wengi wenye elimu na ujuzi bila kazi kwa muda mrefu.
Matiko alisema changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi ni kukosekana kwa dhamana zinazotambulika na benki pamoja na taasisi za fedha, jambo linalowafanya washindwe kupata mikopo hata wanapokuwa na mawazo ya biashara na ubunifu wa miradi ya uzalishaji.