Rais Samia atengua uteuzi wa Diwani Athumani

Muktasari:

  • Rais Samia amemwondoa Diwani Athumani katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Ikulu baada ya kudumu katika nafasi kwa siku mbili tangu alipoteuliwa Januari 3, 2023 akitokea Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Ikulu, Kamishna Diwani Athumani uliodumu kwa siku mbili baada ya kuteuliwa akitokea Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Kamishna Diwani aliteuliwa Januari 3, 2023 kuwa Katibu Mkuu wa Ikulu, akitokea katika wadhifa wa Mkurungezi Mkuu wa TISS, nafasi aliyohudumu kwa siku 1,210 tangu alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Januari 5, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, imeeleza kuwa nafasi ya Diwani imechukuliwa na Mululi Mahendeka aliyekuwa ofisa mwandimizi wa Ofisi ya Rais, Ikulu.

Kabla ya kushika nafasi hizo, Kamishna Diwani aliwahi kuwa msaidizi au mpambe wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) wa zamani, Omary Mahita. Baadaye aliteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya.

Pia, Diwani aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, nafasi alizohudumu kwa nyakati tofauti katika Serikali ya awamu ya tano.