VIDEO: Rais Samia apangua Ikulu, Idara ya usalama wa Taifa

Rais Samia Suluhu Hassan akitoa taarifa  ndogo ya mabadiliko ya nafasi za Uongozi katika Serikali,  Ikulu jijini Dar es Salaam Januari 3, 2023. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wanne akiwemo Said Hussein Nassoro kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akichukua nafasi ya Kamishna Diwani Athuman.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wanne akiwemo Said Hussein Nassoro kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akichukua nafasi ya Kamishna Diwani Athuman.

Awali, Nassoro alikuwa naibu mkurugenzi mkuu na mkurugenzi wa shughuli za ndani wa idara hiyo.

Katika mabadiliko hayo aliyoyatangaza leo usiku, Januari 3, 2023, Rais Samia amemteua Diwani kuwa Katibu Mkuu-Ikulu akichukua nafasi ya Moses Kusiluka ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Diwani ambaye ni Kamishana wa Jeshi la Polisi, amehudumu nafasi hiyo kwa siku 1,210, tangu alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli Septemba 12 mwaka 2019.

Alishika nafasi hiyo kutoka kwa Dk Modestus Kipilimba ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia.

Kabla ya Diwani kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa alikuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Panga pangua hiyo ya Rais Samia ambaye amesema ataendelea kuifanya imemhusisha aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ambaye ameteuliwa kwenda New York nchini Marekani kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN).

Rais Samia apangua Ikulu, Idara ya usalama wa Taifa

Balozi Kattanga ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa katibu mkuu kiongozi Machi 31, 2021, alichukua nafasi ya Dk Bashiru Ali ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa.
Kattanga aliteuliwa kushika wadhifa huo kutoka kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan na sasa anakwenda kuchukua nafasi ya Profesa Kennedy Gaston.

Akitoa sababu za kumrejesha nchini Profesa Kennedy, Rais Samia amesema katika mkutano wa Bunge wa Novemba mwaka jana kulikuwa na mjadala mzito wa matumizi ya fedha na madaraka katika ofisi mbalimbali za kibalozi na ulimwenguni na Serikali inazifanyia kazi dosari hizo.

Amesema, “nimeamua kufanya mabadiliko katika ofisi yetu ya New York kulikokuwa na mwakilishi wetu wa kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN), ofisi hii ni muhimu kwa nchi yetu kwa kuwa ndio inayotuwakilisha kwenye mambo yote yanayojadiliwa na mataifa na taasisi za kimataifa pale makao makuu.

“Kwa msingi huo, ofisi yetu ya New York inahitaji mwanadiplomasia mahiri anayejua siasa za kimataifa, mzalendo kwa nchi yake na mtulivu wa hekima na busara, hivyo nimeamua kumrudisha nyumbani Profesa Kennedy,” alisema