Rais Samia atengua uteuzi wa Gekul

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Pauline Gekul.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus, iliyosambazwa kwa vyombo vya habari leo Jumamosi Novemba 25, 2023; haikueleza sababu za uamuzi huo.
Gekul ambaye ni Mbunge wa Babati Mjini, kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Disemba 5, 2020; chini ya uongozi wa Hayati John Magufuli.
Hata hivyo, Machi 2021, Rais Samia alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, nafasi aliyodumu hadi Februari 23, 2023 aliteuliwa kuwa Naibu wa Wizara ya wa Wizara ya Katiba na Sheria.
Kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi CCM, Gekul aliwahi kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Manyara, pia Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Kanda ya Kaskazini waliotokana na chama hicho.
Hata hivyo Oktoba 2018, Gekul alijivua uanachama wa Chadema, na kujiuzulu nafasi zote za uongozi alizokuwa nazo na kujiunga na CCM, huku akitaja sababu ya fanya hivyo kuwa ni Chadema kuwabebesha wabunge mzigo wa ujenzi wa chama.