Gekul ajibu madai ya kudhalilisha kijana

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Muktasari:

  • Hussein Abrima, Katibu wa mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul ametoa ufafanuzi wa madai yaliyosambaa mtandaoni akisema ni ya kimkakati.

Dar es Salaam. Wakati makundi mbalimbali yakimjia juu Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul kwa madai ya udhalilishaji, mwanasiasa huyo kupitia katibu wa ofisi yake, ametoa ufafanuzi akigusia madai ya kuwapo imani za kishirikiana na ushindani wa kibiashara.

Ufafanuzi huo awali ulitolewa na Hussein Abrima, katibu wa mbunge huyo na ulisambaa kwenye mitandao ya kijamii. Awali Gekul alipotafutwa alielekeza atafutwe katibu wake.

Alipotafutwa katibu huyo leo Jumamosi Novemba 25, 2023 kwa njia ya simu ya mkononi kuthibitisha ufafanuzi huo, alikiri kuandika taarifa hiyo.

Hata hivyo, amesema walishauriana kuifuta kutokana na shauri kuwa mikononi mwa polisi.

“Kuna ushauri ulitolewa nikaufuta kwa sababu jambo lipo polisi ndiyo maana tuliifuta hiyo taarifa kwenye mtandao wa Whatsapp. Polisi wanaendelea na uchunguzi,” amesema.

Kabla ya katibu huyo kutoa ufafanuzi na kuufuta, kupitia mitandao ya kijamii kumekuwa na video inayomuonyesha kijana aliyetajwa kwa jina la Hashimu Ally akidai kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kundi la vijana kwa maelekezo ya Gekul, ambaye alikuwapo eneo la tukio.

Ally anadai Gekul aliamuru aingiziwe chupa sehemu ya haja kubwa au ampige risasi kwa madai alitumwa kimkakati kwenda Hoteli ya Paleii Lake View Garden inayodaiwa kumilikiwa na Gekul.

Tangu kuanza kusambaa kwa video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, wanasheria, watetezi wa haki za binadamu na wadau mbalimbali, wametaka kiongozi huyo wa umma kuwajibika mara moja au mamlaka za juu kumchukulia hatua za kinidhamu ikiwamo kutengua uteuzi wake.

Kupitia mtandao wa X, wakili wa kujitegemea Peter Madeleka aliandika: “Kitendo cha kishetani alichofanyiwa Hashimu Ally Philemoni kuingiziwa chupa sehemu ya haja kubwa, siyo siasa. Tunataka wote wanaotajwa kuhusika na ushetani huu, wawajibishwe bila kujali vyeo vyao.”

Mwanasiasa aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kupitia ukurasa wake wa X ameomba haki itendeke.

Maria Sarungi, ambaye ni mwanaharakati kupitia mtandao huo ametaka kufanyike uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.


Taarifa iliyofutwa

Taarifa ya Abrima, katibu wa mbunge huyo aliyoitoa na baadaye kuifuta kwenye mtandao ilidai wameona video ndogo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimtuhumu Gekul kwa matukio mbalimbali ambayo hayana ukweli wowote.

Kupitia taarifa hiyo, inadaiwa kinachoendelea ni mbinu za wahutumiwa kutaka kuwatoa watu kwenye ajenda ya msingi ya tuhuma zao zinazowakabili.

Taarifa imedai ofisi ya mbunge imefuatilia kwa kina jambo hilo na kubaini Hashimu Ally alikuwa mtumishi wa Paleii Like View  Garden na alikuwa akijitambulisha kwa jina la Jonathan, baada ya kuacha kazi eneo jingine (jina limehifadhiwa) linalodaiwa kuwa na ushindani wa kibiashara na Paleii Lake View Garden.Inadaiwa maeneo hayo mawili yanafanya kazi inayofanana ya biashara ya chakula.

“Novemba 11, 2023 saa nne asubuhi ndugu aliyejitambulisha Maiko alienda Paleii akiomba kazi kwa madai alipokuwa akifanya kazi awali (inatajwa jina) amefukuzwa. Kijana huyo aliposikilizwa na uongozi wa Paleii, alielezwa hakuna uwezekano wa kupata kazi jambo ambalo hakukubaliana nalo na kutaka kuonana na Pauline Gekul mwenyewe ili aweze kumueleza yaliyomsibu,” imedai sehemu ya taarifa hiyo.

Inadaiwa baada ya kiongozi huyo kurejea akitokea msibani mkoani Arusha, alipata taarifa ya kijana huyo kuomba kazi na kuhusika na vitendo vya kishirikina (kuchota mchanga) ndipo alipompa nafasi ya kumsikiliza.

“Wakati wa maelezo ya kijana huyo, ilibainika alitumwa kimkakati kuchota mchanga yeye na vijana wenzake wawili kwa lengo la kupeleka ukatumike kishirikina,” imedai taarifa hiyo.

Inadaiwa kijana huyo alikiri kuwapo mganga aliyekuwa akisubiri mchanga huo  katika hoteli moja akitokea Iringa.

Taarifa inadai kijana huyo alimtaja mfanyakazi wa Paleii aliyekuwa akifanya naye katika eneo lake la awali anayejitambulisha kwa jina la Jonathan, lakini jina lake halisi ni Hashimu.

Inadaiwa katika taarifa hiyo kwamba mdogo wa mmiliki wa hoteli hiyo anahusika katika kusambaa kwa taarifa zilizozua taharuki juu ya jambo hilo.

Aidha, katibu huyo amedai suala hilo limepelekwa kimrengo wa kisiasa na kuchafua hadhi ya mbunge na taasisi nyingine za chama na Serikali.

“Ndugu wananchi na wakazi wa Babati Mjini kwa kuwa jambo hili lipo kwenye vyombo ya dola, ofisi inawaomba kuendelea kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi linaendelea kushughulikia jambo hili ili kutoa haki kwa pande zote mbili,” imeeleza taarifa hiyo.


Madai kwenye video

Kupitia video hiyo Kijana huyo anawaomba wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kumsaidia apate haki yake, akidai Novemba 11, 2023 aliitwa na mwajiri wake kwenye chumba cha wageni maalumu.

Anadai alimkuta Gekul, katibu wake, mtu mwingine ambaye hakumtaja na kijana mmoja  aliyekuwa amepiga magoti, hivyo naye alitakiwa apige magoti.

Kijana huyo anadai alishutumiwa kwamba aliweka dawa eneo la kazi na kuweka sumu kwenye chakula.

Anadai alikana, ndipo akatajiwa jina la aliyemtuma. Hata hivyo, anadai aliendelea kukana na simu yake ilikaguliwa na hakuna kilichobainika.

Anadai walivuliwa nguo na kuingiziwa chupa, pia walitishiwa kuuawa kwa bastola.

“Aliita polisi wakaja kutuchukua tukakaa polisi siku nne tunahojiwa kuanzia saa mbili mpaka saa nane, siku ya tatu nikaitwa nikaulizwa tena ulitumwa nikakana nikarudishwa polisi,” amedai.

Anadai siku ya nne alitoa mawasiliano ya baba yake kwa ajili ya dhamana, na alipotoka alichukua fomu ya polisi kwa ajili ya matibabu (PF3) kutokana na maumivu aliyopitia.