Rais Samia atengua uteuzi wa RC Simiyu, Kihongosi kumrithi

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda.

Muktasari:

  • Katika uteuzi alioufanya Rais Samia Suluhu Haasan ameigusa tena ofisi yake

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda, huku akiteua viongozi wanne na kuigusa tena ofisi yake.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumanne Juni 11, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga inasema nafasi ya Dk Nawanda inajazwa na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi.

Dk Nawanda alikuwa kwenye nafasi hiyo tangu Julai 2022.

Kihongosi amekuwa kuwa Mkuu wa wilaya za Urambo, Iramba na Arusha.

Pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM) na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.

Rais Samia amemteua Elias Mwandobo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Momba. Kabla ya uteuzi huo, Mwandobo alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu.

Juni 6, 2024 Rais Samia alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, akiigusa ofisi yake kwa kuteua watendaji wanne katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Miongoni mwa viongozi waliotoka katika ofisi ya Rais ni Zuhura Yunus aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Felister Mdemu aliyekuwa msaidizi wa Rais, Maendeleo ya Jamii.

Wengine ni Petro Itozya aliyekuwa msaidizi wa Rais Siasa na Nehemia Mandia aliyekuwa msaidizi wa Rais upande wa sheria.

Katika uteuzi uliofanyika leo, Rais Samia amemteua Christopher Magala kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, akichukua nafasi ya Stephen Mwakajumilo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Mwakajumilo aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo Septemba 23, 2023. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Mbali na hayo, taarifa ya Ikulu ya leo Juni 11, 2024 inaeleza George Herbert ameteuliwa kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo alihudumu nafasi ya Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani.