Mabadiliko Ofisi ya Rais yalivyowaibua wadau

Muktasari:

  • Katika mabadiliko ya Juni 6, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan amebadilisha wasaidizi wake wanne wa Ikulu.

Dar es Salaam. Mabadiliko aliyoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan Juni 6, 2024 yamewaibua wadau na wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala, baadhi wakishauri uchunguzi wa kina uwe unafanyika kwa wateule wa Rais, ili kuepusha mabadiliko ya mara kwa mara.

Wamesema Ofisi ya Rais inatakiwa kuwa na utulivu, hasa wakati huu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.

Katika mabadiliko hayo, Rais amebadilisha maofisa wanne wa Ikulu, akiwamo Zuhura Yunus aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Felister Mdemu aliyekuwa msaidizi wa Rais, Maendeleo ya Jamii, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu anayeshughulikia masuala ya jinsia na wanawake.

Wengine ni Petro Itozya aliyekuwa Msaidizi wa Rais Siasa na Nehemia Mandia aliyekuwa msaidizi wa Rais upande wa sheria walioteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na Jaji wa Mahakama Kuu mtawalia.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka Juni 6, imeeleza kuwa Rais amefanya uteuzi huo katika kuboresha utendaji kazi.

Akijadili mabadiliko hayo, mwanahabari mkongwe Absalom Kibanda amesema pamoja na madaraka aliyonayo Rais Kikatiba, bado madaraka hayo yanatakiwa yalete manufaa.

“Kwa sasa wakati ambao Rais ni mwenyekiti wa CCM na kwa kipindi ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi, mabadiliko ya mara kwa mara yanaweza kuleta shida,” amesema.

Kibanda akizungumzia kuondolewa kwa Zuhura Yunus, Ikulu amesema kwa nafasi aliyopelekwa inaonekana ni kupandishwa cheo, lakini kwa namna nyingine ni kushushwa.

“Kwa sisi wanahabari Zuhura alikuwa kama taswira ya Rais na hata taarifa za mabadiliko anayofanya, tulizoea kuziona kama ni za Zuhura.”

“Kama Rais angekuwa anamaliza muda wake anaondoka na akamteua Zuhura kwenye nafasi hiyo, tungesema amempandisha cheo, lakini kwa wakati huu, ghafla tu amemhamisha, basi kutakuwa hakujakaa sawa,” amesema.

Alizungumzia ufanisi wa kazi, Kibanda amesema inawezekana kuna mambo hayakwenda sawa kwenye ziara ya Rais Samia nchini Korea Kusini iliyomalizia jana Juni 6, 2024.

Maoni hayo yameungwa mkono na mwanasheria mkongwe na mtetezi wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo -Bisimba akisema, Rais anatakiwa kuwa na utulivu na timu yake.

“Kwa sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, kuwaondoa watu wanne katika ofisi yake hakuleti picha nzuri.

“Rais anapoteua watu unatakiwa ufanyike uchunguzi wa kutosha, lakini haya mabadiliko ya mara kwa mara inaonekana bado hajapata watu wa kutulia. Mtu anapoteuliwa anapewa nafasi aonekane na anafundishwa kazi,” amesema.

Ameshauri pia Ofisi ya Rais kuwa na mawasiliano na mamlaka nyingine ili kuhakikisha watu wanaoteuliwa wanakuwa tayari kwa kazi.

Katika mtazamo tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus amesema huenda mabadiliko ya mara kwa mara yanasababishwa na kutokuwapo kwa ufanisi.

“Kwanza, inawezekana baadhi yao wameshindwa kuendana na falsafa yake ya urais. Pili, inawezekana lile tatizo alilokuwa analiongelea mara nyingi la taarifa za Ikulu au za Rais kuvuja likawa linahusu baadhi yao.”

“Tatu, kuna uwezakano mkubwa amebaini kuwa anahitaji kujipanga zaidi kisiasa kwa uchaguzi mkuu wa mwakani, hivyo kupunguza watendaji ambao wana ukada zaidi na kuanza kufanya kazi na wataalamu au kinyume chake, kwamba anahitaji kufanya kazi na wasaidizi watakaomsaidia zaidi kisiasa,” amesema.

Kuhusu Zuhura Yunus kutodumu Ikulu, amesema inawezekana kuondoka kwake kumelenga kumtengenezea njia ya kuendelea kupanda ngazi katika nafasi mbalimbali za Serikali na kumzoesha mfumo wa utendaji serikalini mapema.

“Ingawa wengine wanaweza kusema ameshindwa kumudu jukumu la kuratibu taarifa zinazohusu ofisi ya Rais. Taarifa zinazomhusu Rais zimekuwa na watoa taarifa wengi mno kipindi hiki, bila ya uratibu mzuri na kusababisha wananchi kutokuelewa kipi ni sahihi na kipi siyo sahihi,” amesema.


Mabadiliko mengine

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Stanslaus Nyongo kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji.

Pia amemteua Amon Mpanju kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu anayeshughukia masuala ya maendeleo ya jamii na makundi maalumu.

Katika taarifa hiyo, Balozi Kusiluka amesema Rais amefanya uteuzi na uhamisho wa wakuu wa wilaya, akimteua Itozya kuwa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Nyangasa amehamishwa kutoka Kisarawe kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa.

Pia Dk Hamis Mkanachi amehamishwa kutoka Wilaya ya Kondoa kwenda kuwa mkuu wa Wilaya ya Urambo na aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Elibariki Bajuta atapangiwa kazi nyingine.

Rais Samia pia amewahamisha makatibu tawala wa wilaya ambao Reuben Chongolo kutoka Wilaya ya Songwe kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi.

Frank Sichwale amehamishwa kutoka Wilaya ya Mufindi kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe.


Wakurugenzi nao wamo

Uteuzi na uhamisho wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri umewagusa Mussa Kitungi ayeteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia; Kalekwa Kasanga kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Shaaban Mpendu ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati na Sigilinda Mdemu kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele.

Rais Samia amemhamisha Upendo Mangali kutoka Halmashauri ya Mji wa Babati kwenda kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga,  Kisena Mabuba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwenda kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, akichukua nafasi ya Mwantum Mgonja ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Teresia Irafay amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwenda kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang'.


Majaji Mahakama Kuu

Rais pia amefanya uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ambao ni Mandia aliyekuwa msaidizi wa Rais upande wa sheria,  Projestus Kahyoza aliyekuwa maibu msajili mwandamizi wa Masijala Kuu ya Mahakama Kuu, Dodoma na Mariam Omary aliyekuwa naibu msajili mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

“Uapisho wa naibu wziri, naibu makatibu wakuu na majaji wa Mahakama Kuu utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye,” amesema Balozi Kusiluka katika taarifa hiyo.