Rais Samia ateta na mabalozi wa Tanzania nchi za nje

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akizungumza na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Nchi za Nje kwa njia ya Mtandao (Video Call) leo Jumatatu, Aprili 22,2024 walipokuwa kwenye mkutano unaojadili kuhusu mkakati wa Diplomasia ya Umma na Tathmini ya Kiutendaji (Retreat) uliofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Muktasari:

  • Rais Samia amesema Tanzania inawategemea sana mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao Ili iweze kusonga mbele kiuchumi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema amechukua hatua mbalimbali ili kuibadilisha Wizara ya Mambo ya Nje iwe ya kisasa zaidi na kuwa na uwezo wa kuitangaza nchi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Aprili 22, 2024 alipokuwa anawahutubia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Mabalozi hao wamekusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya siku nne kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje iliyoanza Aprili 21 na inatarajiwa kukamilisha Aprili 24 mwaka huu.

Samia amesema Tanzania inawategemea sana mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao Ili iweze kusonga mbele kiuchumi.

Akizungumzia mabadiliko aliyoyafanya amesema yamelenga kuifanya nchi iendelee kuheshimika na kuwa na ushawishi zaidi duniani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma ya wakati wa harakati za ukombozi na baada ya ukombozi.

Akitaja miongoni mwa hatua alizochukua ni pamoja na kuteua Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, kuanzisha Idara ya Diplomasia ya Uchumi, kusaini mikataba ya Kuzuia Utozaji wa Kodi mara Mbili na Kulinda Vitega Uchumi na nchi mbalimbali duniani.

“Pia, kuridhia mkakati wa uendelezaji wa majengo ya ofisi za mabalozi na makazi na mchakato wa uboreshaji wa Sera ya Mambo ya Nje na Hadhi Maalumu kwa raia wenye asili ya Tanzania wanaoishi Nje ya nchi ambao umefikia hatua nzuri,” amesema Samia.

Amewasihi mabalozi kuwa jicho la Tanzania kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani.

Akizungumzia misingi sita ya Sera ya Mambo ya Nje ambayo Tanzania inaisimamia tangu ilipopata uhuru, Samia amesema ni vyema wakaendelea

kulinda uhuru wa kujiamulia, kuheshimu mipaka ya nchi, kulinda uhuru, haki za binadamu na usawa wa kidemokrasia, kudumisha ujirani mwema, kuunga mkono Umoja wa Mataifa (UN), kuendeleza mshikamano wa Umoja wa Afrika na kuunga mkono Sera ya kutofungana na Upande Wowote.

“Katika Maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje yanayoendelea napendekeza kuongeza msingi wa saba ambao ni kulinda masilahi ya kiuchumi na maadili ya watu. Katika msingi huu, nasisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi yetu na Utamaduni wake,” amesema Samia.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo madini adimu, hivyo endapo nchi haitakuwa na mpango madhubuti wa kulinda rasilimali hizo na kunufaika nazo, basi badala ya kuwa fursa kwa Taifa zinaweza kugeuka na kuwa janga.

“Pia, ni umuhimu wa kulinda utamaduni wetu kwa kuwa kuna juhudi za makusudi zinazoendelea duniani za kulazimishwa tamaduni zilizo kinyume na maadili yetu,” amesema Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewapongeza mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kwa kazi inayoonekana ikiwemo kuongezeka kwa masoko ya bidhaa za Tanzania, biashara, uwekezaji, utalii na teknolojia nchini.