Rais Samia ‘kuwafunda’ mabalozi wa Tanzania nje ya nchi

Rais Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
Mkutano huo uliopangwa kufanyika Zanzibar kuanzia Novemba 14 – 21, 2022 ni wa kwanza tangu Rais Samia alipoingia madarakani na unabeba kaulimbiu isemayo: “Mwelekeo Mpya Katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi”.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kukutana na mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.
Mkutano huo uliopangwa kufanyika Zanzibar kuanzia Novemba 14 – 21, 2022 ni wa kwanza tangu Rais Samia alipoingia madarakani na unabeba kaulimbiu isemayo: “Mwelekeo Mpya Katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi”.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 12, 2022 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.
Dk Tax amesema lengo la mkutano huo ni kutoa fursa kwa mabalozi na watendaji wa wizara wanaoshiriki katika uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kupokea maelekezo ya Rais Samia pamoja na viongozi wengine kuhusu mwelekeo wa Serikali.
Amesema mkutano huo pia unalenga kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi, kuainisha changamoto katika utekelezaji wa majukumu na kuja na mikakati madhubuti ya namna ya kuzitatua.
“Mkutano huu ni fursa kwa Tanzania kuandaa mikakati ya pamoja ya namna ya kujiweka sawa (repositioning) ili kuhakikisha Taifa linanufaika ipasavyo kutokana na fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo ya uwakilishi.
“Mabalozi wetu wote kutoka balozi zote 45 wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi watakuwepo nchini na moja ya majukumu waliyoelekezwa ya kufanya wakiwa hapa nchini ni kujulisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Dk Tax.
Ameongeza kwamba baada ya mkutano huo balozi za Tanzania zitajipanga upya ili kuongeza ubunifu katika kuiletea nchi maendeleo na kufikia azma ya Serikali ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.
Dk Tax amesema balozi za Tanzania zimefanya kazi nzuri na ya kuridhisha ya kutafuta wawekezaji, masoko ya bidhaa zetu, misaada na mikopo nafuu ya maendeleo na kuvutia watalii kuja nchini.
Ziara hizo zimeratibiwa vizuri na balozi za Tanzania nje ya nchi zimekuwa na mafanikio makubwa katika diplomasia ya Tanzania
Amesema, katika siku hizo wamealika wadau mbalimbali wa Sekta ya umma na binafsi kuongea na mabalozi masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao.