Rais Samia awateua tena Dk Mafumiko, Wassira
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya uteuzi wa viongozi na watendaji wa serikali na taasisi zake ambapo leo Machi 25, 2023 amewateua viongozi wawili ambapo ni Mwenyekiti wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wassira na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wawili wa taasisi za umma kwa kuwaongezea muda katika nafasi zao akiwamo Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko ambaye ameongezewa miaka mingine mitano.
Dk Mafumiko aliteuliwa kuongoza taasisi hiyo Aprili 3, 2018 na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli akitokea Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ambako alikuwa Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 25, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, uteuzi wa Dk Mafumiko kwa kipindi kingine cha miaka mitano utaanza Aprili 3, 2023.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko.
“Rais Samia amemteua Dk Fidelice Mafumiko kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia Aprili 3, 2023,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.
Rais Samia amemteua pia Stephen Wassira kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kwa kipindi cha pili cha miaka minne.
Wassira ambaye amekuwa mbunge na waziri katika awamu tofauti, ameongoza bodi ya chuo hicho kwa miaka minne iliyopita na sasa Rais Samia amemuongezea muda wa kipindi cha pili cha miaka minne mingine.
Stephen Wasira ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA).
“Rais Samia amemteua Stephen Wassira kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kwa kipindi cha pili cha miaka minne baada ya kipindi cha kwanza kumalizika,” inaeleza taarifa hiyo.