Rais Samia kufanya ziara siku nne Mara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani hapo itakayoanza Februari 4, 2022. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne mkoani Mara ambapo pamoja na mambo mengine atahudhuria maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma.
Musoma. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne mkoani Mara ambapo pamoja na mambo mengine atahudhuria maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumanne Februari Mosi 2022 Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi Rais Samia atatembelewa na kukagua miradi mbalimbali ikiwamo ya sekta za afya, maji na utawala yenye thamani ya zaidi ya Sh126.21 bilioni.
Amesema kuwa Rais anatarajiwa kuwasili mkoani Mara Februari 4 ambapo Februari 5 akitarajiwa kuongoza maadhimisho ya miaka 45 ya CCM na baada ya maadhimisho hayo atatembelea mradi wa ujenzi wa hospitali ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.
Hapi amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa hospitali ya Kwangwa ulioanza mwaka 1975 umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake huku Serikali ikitarajia kutumia zaidi ya Sh41.49 bilioni.
Amesema kuwa Miradi mingine ni pamoja na wa Mugango- Kiabakari na mradi wa chujio la maji mjini Bunda.
"Mradi wa Mwisho utakuwa ule wa ujenzi wa ofisi za makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Butiama mradi ambao utagharimu zaidi ya Sh3.26 bilioni na upo asilimia 77 ya utekelezaji wake pia atapata fursa ya kutembelea kaburi la baba wa Taifa Mwalimu Nyerere pale Mwitongo" amesema Hapi.