Rais Samia, Mbowe wateta Ikulu

Muktasari:

  • Saa chache baada ya kutoka gerezani mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam. Saa chache baada ya kutoka gerezani mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa na picha ya kurugenzi ya mawasiliano Ikulu imeaanza kusambaa mitandao ya kijamii kuanzia leo Ijumaa Machi 4, 2022 saa nne usiku ikiwa ni takribani saa tano tangu Mbowe kutoka gerezani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kufuta kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake watatu.

Taarifa hiyo ya Ikulu inaeleza kuwa Rais Samia amezungumzia kuhusu umuhimu wa kushirikiana ili kujenga Tanzania kwa kuaminiana na kuheshimiana kwa misingi ya haki.

Kwa upande wake Mbowe amemshukuru Rais Samia kwa kuonyesha kujali huku akikubali kuwa msingi mkubwa wa kujenga Tanzania ni kusimama katika haki.

Katika taarifa hiyo, Mbowe amenukuriwa akisema kuwa wamekubaliana kufanya siasa za kistaarabu na kiungwana na kwamba yupo tayari kushirikana na Serikali kuleta maendeleo.