Rais Samia: Mwananchi kwanza, sisi huku juu baadaye

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amezungumza na wakazi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ambapo ameelezea mwenendo wa Serikali yake hivi sasa na jinsi inavyoboresha sekta ya kilimo.

Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mwenendo wa Serikali ya awamu ya sita hivi sasa ni kushusha fedha kwa wananchi.

Samia ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 22, 2022 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Bicha Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma wakati akiwa njiani kwenda mkoani Manyara.

Amesema kazi ya kuleta maendeleo ni kubwa lakini pia mapato ni madogo hivyo yanapopatikana wanayagawanya.

“Lakini tumejitahidi sana kushusha fedha chini kwa wananchi kwenye sekta mbalimbali na huu ndio mwenendo wetu sasa, mwananchi kwanza, sisi huku juu baadaye tutajijua wenyewe tutakavyoishi lakini kwanza mwananchi,” amesema.

Amesema ndio maana wameshusha fedha nyingi chini ili ziende kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, Rais Samia amesema mabwawa ya maji yatakayojengwa kwa ajili ya kukinga maji ya mvua yataanza kutumika katika misimu ijao (mvua) kwasababu magari hayo ndio yamegaiwa mwaka huu.

“Pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mmesikia tumegawa magari ya kuchimba mabwawa na Dodoma imepata mitambo hiyo kule kote kwenye uhaba wa mvua mbwawa yatakwenda kuchimbwa,” amesema.

Kuhusu ujenzi wa madaraja, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wana madaraja matatu wanajenga ikiwemo la Mwigiri na Karema.

Amesema daraja la Mwigiri wamefanya usanifu kwa Sh470 milioni na kwamba katika bajeti ya 2022/23 wametenga Sh600 milioni kwa ajili ya usanifu wa kina kabla ya kuanza ujenzi.

Kuhusu daraja la Karema, amesema tayari kazi ya usanifu imekamilika na wako katika hatua ya kumfuta mkandarasi ambapo katika bajeti ya mwaka 2022/23, wametenga Sh600 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi utakaokamika baada ya mwaka mmoja.

Aidha, amesema ujenzi wa barabara inayounganisha mikoa mitatu ya Dodoma, Tanga na Singida ambapo ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi ili ujenzi wake uweze kuanza.

“Tunaamini kuwa itabadilisha maisha ya wananchi wa Kondoa na maeneo mengine itakapopita barabara hii,”amesema.