Rais Samia: Tanzania kuna wagonjwa wa corona

Rais Samia: Tanzania kuna wagonjwa wa corona

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema tayari kuna wagonjwa wa Covid-19 wamebainika nchini kwenye wimbi la tatu la ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona na  kuwataka viongozi wa dini kuwaelekeza waumini kuchukua tahadhari.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema tayari kuna wagonjwa wa Covid-19 wamebainika nchini kwenye wimbi la tatu la ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona na  kuwataka viongozi wa dini kuwaelekeza waumini kuchukua tahadhari.

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akizungumza na Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwenye makao yao makuu yaliyopo Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kutoa taarifa za kuwepo kwa maambukizi ya corona nchini kwani mara ya mwisho kutoa takwimu za ugonjwa huo ilikuwa Mei, 2020.

Amesema kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba ni muhimu kwa watu kuendelea kutumia kila kinachoelekezwa kuwa kinga ya maradhi hayo ili kuliepusha taifa na vifo.

“Nafahamu kuwa kanisa tangu mwanzo limekuwa na msimamo thabiti wa kupambana na ugonjwa huu.

“Tumeingia kwenye wimbi la tatu la ugonjwa huu na ishara ndani ya nchi zinaonekana, tayari tuna wagonjwa ambao wameshaonekana katika wimbi hili,” amesema.

Rais Samia ameeleza kuwa alipotembelea Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam hivi aliwakuta wagonjwa wenye tatizo hilo.

“Niwasisitize kuwa hili jambo bado lipo tusijiachie na tuwaombe viongozi wa dini mlisemee kwa sauti kubwa kwa waumini wenu ili kujiepusha na vifo vya makundi. Pia tumuombe Mungu atuepushe na janga hili,” ameeleza Rais Samia.