Rais Samia: Vijana wanahangaika na supu ya pweza, vumbi la kongo

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika utafiti wa kwanini vijana balehe wanamatizo ya lishe ili kuepuka kuwa na Taifa goigoi.


Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika utafiti wa kwanini vijana balehe wanamatizo ya lishe ili kuepuka kuwa na Taifa goigoi.

Samia ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 30, 2022 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe.

“Watoto balehe hebu tufanye utafiti, tunakosea wapi, kwanini tunakuwa na lishe ndogo. Kwanini kunakuwa na hizo gaps (mianya). Kwanini tunakuwa na watoto wazuri kiafya, Je ni masuala ya mitindo? Nataka sijui slim, nataka sijui niwe kilo ngapi, nataka sijui mbavu ikae vipi kuna nini hasa kwanini wawe hivi”amehoji Samia.



Amesema wakati wakutafuta watoto vijana hao wanahangaika mara kunywa supu ya pweza na kwamba kuna tatizo ambalo wanalijua lakini wanalificha.

“Watafiti fanyeni tafiti, tuna tatizo, kwasababu halisemwi ni siri linawaumiza zaidi vijana wetu, mara haya ninayoyataja, mara vumbi la Kongo, mara kitu gani lakini tatizo kubwa liko kwenye lishe. Sasa watafiti fanyeni tafiti vijana wetu waweze kuzaa watoto wenye afya,”amesema.

Amesema jamii hiyo ni ya watu wote waweze kufanyia kazi na kwamba wakiacha hilo liendelee wanaenda kuwa na Taifa goigoi ambalo lina watu lakini si raslimali watu ambao ni mzigo kwa Taifa na si wazalishaji kwa ajili ya Taifa.

“Tutafika mahali hatujui mume nani, mke nani. Kwa hiyo twendeni tukasimamie hilo…Wavulana mnaonekana mmevaa suti lakini kuna vigenge vya udongo (vumbi) la kongo chungu mzima, Amos (Mkuu wa Dar es Salaam-Amos Makala) unanitazama huko ndio kunasifika kwa chipsi,”amesema