Rais Xi Jinping amlilia Magufuli

Rais Xi Jinping amlilia Magufuli

Muktasari:

  • Rais wa China,  Xi Jinping amesema amepokea kwa mshtuko  kifo cha marehemu John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 akimuelezea kuwa alikuwa kiongozi aliyelinda hadhi ya Tanzania.

Dar es Salaam.  Rais wa China,  Xi Jinping amesema amepokea kwa mshtuko  kifo cha marehemu John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 akimuelezea kuwa alikuwa kiongozi aliyelinda hadhi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Jinping amemuandikia barua Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan  akimpa pole za kifo cha mwanamajumui huyo wa Afrika huku akimpongeza kuapishwa kuwa rais.

Kwa mujibu wa barua hiyo, rais Jinping amesema, “mimi binafsi, Serikali ya China tunatoa salamu za rambirambi kwa familia, Serikali na Watanzania  kufuatia kifo hicho.”

Rais Jinping amesema enzi za uhai wake Mgufuli aliyekuwa maarufu Tanzania na Afrika aliwaongoza Watanzania kulinda hadhi ya nchi yao kuingiliwa na mataifa huku akiwaletea maendeleo  yanayoendana na hali halisi ya Tanzania.

Amesema Magufuli alishiriki pia kutoa mchango chanya ulioendeleza urafiki kati ya China na Tanzania sanjari na Afrika.

“Kifo cha Rais Magufuli ni pigo kwa Watanzania na pia China imepoteza rafiki wa kweli,” amesema kiongozi huyo wa China.

Taarifa hiyo inamnukuu Rais Jinping akisema anajivunia urafiki wa muda mrefu na Tanzania huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano  kukuza mahusiano hayo kwa kiwango cha juu kwa maslahi mapana ya pande hizo mbili.