RC Chacha awaongoza mamia kuuaga mwili wa RPC Abwao Tabora
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, likiwa katika viwanja vya FFU Tabora.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amewaongoza mamia ya viongozi na wananchi wa mkoa huo kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao, katika Uwanja wa FFU mjini Tabora.
Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amewaongoza mamia ya viongozi na wananchi wa mkoa huo kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao, katika Uwanja wa FFU mjini Tabora.
Akizungumza katika Misa Takatifu ya kuuaga mwili wa kamanda huyo, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Josephat Bududu ametoa rai kwa wananchi kuiga mfano wa maisha ya kumcha Mungu aliyokuwa akiyaishi Abwao.
Amesema daima alikuwa mtu wa ibada na aliyependa kushirikiana na kila mtu katika hali zote.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, akizungumza wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, iliyofanyika katika uwanja wa FFU, Tabora mjini.
"Na kamanda huyu alikuwa kiongozi mahiri aliyependa watu na alikuwa mtu wa hekima na busara, ni soma alilotuachia,” amesema askofu huyo msaidizi.
Akizungumza baada ya misa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Chacha amesema mkoa huo utaendelea kuwa salama wakati wote kama ulivyokuwa enzi za uhai wa Kamanda Abwao.
Amesema marehemu Abwao hakuwa askari tu, bali kiongozi aliyetambua wajibu wake na mchapakazi aliyejituma katika majukumu yake, huku akidumisha ushirikiano mkubwa kati ya Jeshi la Polisi na wananchi wa Tabora.
“Kamanda Abwao katika maisha yake ya utendaji kazi hapa Tabora, ni hadithi tosha ya kujifunza namna bora ya namna alivyokuwa anashirikiana na makundi ya watu wa aina zote, licha ya kuwa alikuwa kiongozi katika eneo la usalama,” amesema RC Chacha.
Amesema Tabora ni mkoa mkubwa wenye idadi kubwa ya watu, hivyo ni wajibu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu huku wakitekeleza majukumu yao ya kila siku, na ndivyo alivyofanya Abwao.
Waombolezaji wakiwa kwenye Ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Richard Abwao.
“Niwatoe hofu wananchi wangu kwamba pamoja na wingi tulionao, si sababu ya kuishi kwa hofu. Tumejipanga kuhakikisha mnaishi kwa amani na hakuna kibaka wala mtu yeyote atakayekuja kusumbua hapa,” amesema.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema jeshi hilo limepoteza kamanda mchapakazi aliyeacha alama kubwa ya ushirikiano na wananchi, jambo lililosaidia kupungua kwa uhalifu mkoani Tabora.
“Sisi tumejifunza mengi, lakini kubwa zaidi ni kuendeleza huduma shirikishi kwa wananchi kwa sababu tumeona mafanikio yake hapa Tabora,” amesema Kamanda Misime.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba amesema kamanda atakayechukua nafasi ya Abwao anatakiwa kuendeleza viwango vya utendaji vilivyowekwa, akisisitiza kuwa wananchi wa Tabora wamezoea huduma bora za ulinzi na usalama.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Ibrahim Mavumbi, amesema Kamanda Abwao alikuwa kiongozi aliyetoa huduma bila ubaguzi wa dini, siasa wala mila, jambo lililowatia moyo wa kuendelea kuuombea amani mkoa huo.
“Tumeondokewa na mtu muhimu sana. Hatuna cha kubishana na mapenzi ya Mungu, tumuombee apumzike kwa amani,” amesema.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Magharibi Kati, Tabora, Elias Chakupewa akimzungumzia kamanda huyo, amesema maisha yake yalikuwa ya manufaa makubwa kwa wananchi wa Tabora, akibainisha kuwa alikuwa mtu wa ibada na mwenye nidhamu ya kazi.
“Alikuwa mtu wa ibada na anayependa dini, na huenda hilo ndilo lililochangia mafanikio yake katika majukumu yake. Apumzike kwa amani,” amesema.