RC Iringa azindua mpango utoaji pembejeo

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amezindua mpango wa utoaji wa pembejeo na elimu kwa wakulima kupitia duka model katika Kijiji cha Kalenga kilichopo Mkoa wa Iringa.
Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amezindua mpango wa utoaji wa pembejeo na elimu kwa wakulima kupitia duka model katika Kijiji cha Kalenga kilichopo Mkoa wa Iringa.
Maduka hayo yatafunguliwa 9 katika Mkoa wa Iringa, lengo likiwa ni kutatua changamoto ya bei kubwa za pembejeo na kuondoa gharama za usafirishaji kutoka kijijini hadi wilayani na kumpunguzia mkulima mzigo na kuongeza tija.
Dendego amezindua duka hilo leo Agosti 19, 2022 ambalo ni uwekezaji wa kampuni ya One Acre Fund katika Kijiji cha Kalenga mkoani hapo na kutoa rai kwa watendaji, viongozi, maafisa kilimo kwa ngazi zote kwenda kusimamia programu hiyo ya ruzuku kwa umakini mkubwa, weledi na kuhakikisha hamna namna yeyote ya udanganyifu.
"Mimi na timu yangu hatutalala kuhakikisha waliosajiliwa kweli ni wakulima na taarifa tulizopokea za maeneo wanayolima niza kwelina mahitaji yaliyobainishwa ya pembejeo ndio yanayotakiwa yeyote atakayeenda kinyume na hapo tutaanza naye.
Nawaagiza maafisa wote kuhakikisha orodha zao ni wakulima," amesema Dendego.
Dendego amesema kuwa ujio wa programu ya duka model ni uwekezaji wa kampuni ya One Acre Fund umeendelea kukua kutoka vijiji 30 mpaka vijiji 113 kutoka Mwaka 2012 na waliweza kuwafikia wakulima 4276 mwaka 2014 lakini sasa wamewafikia wakulima takribani 100,000 kwa mwaka 2021/2022.
Mkurugenzi wa Kampuni ya One Acre Fund, Amar Hamad amesema uzinduzi wa maduka hayo ni moja ya kuwasaidia wakulima katika kuongeza tija katika uzalishaji mazao.
Hamad amesema wanaishukuru serikali kwa mchango endelevu kwani tangu kuanza kwa programu hiyo waliamza na vijiji 7 katika vijiji vya Kalenga na Magulilwa huku wakihudumia wakulima 1,148 na leo hii wanahudumia wakulima zaidi ya 160,000 katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini.
"Programu hii ya maduka itaenda bega kwa bega na programu ya msingi ya kutoa mikopo ya pembejeo, itaweza kuwahudumia wakulima wenye pesa taslimu na wakulima wanaohitaji mkopo tunayofuraha kuzindua maduka mkoani hapa ili kuwafikia wakulima wengi zaidi," amesema.
Amesema katika msimu ujao wa kilimo wa mwaka 2021/2022 wameagiza tani 15,000 za pembejeo na kutarajia kusambaza katika vijiji 400 na maduka 40 Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwaka huu.
Mmoja wa wakulima kutoka Kalenga, Zakia Malamy amesemà uwepo wa duka hilo utawasaidia kupata huduma za pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu tofauti na awali walikuwa wananunua kutoka maduka binafsi kwa bei kubwa.
"Duka hili litatusaidia kupunguza gharama za usafirishaji na tutanunua karibu na maeneo yetu na tutakuwa na uhakika wa kupata mbolea kwa kipindi cha msimu mzima wa kilimo na kwa wakati, pia tutapata ushauri na tutanunua mbolea kwa mkopo na pesa taslimu," amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo amesema wilaya ya Iringa ina eneo la hekari 479,158 liñalofaa kwa kilimo huku linalolimwa ni ekari 319,438 na wilaya ikiwa na wakulima 81,060 pekee.
Moyo amesema kuwa malengo ya uzalishaji ya msimu huu wa 2022/23 ni kulima hekari 200,219 kwa mazao ya chakula na hekali 290,256 za mazao ya biashara huku mahitaji ya pembejeo kwa msimu wa 2022/23 ni tani 110,341 za mbolea na tani 3,357 za mbegu.