RC Kagaigai awataka viongozi wa dini kuliombea Taifa
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Stephen Kagaigai amewataka waumini na viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Stephen Kagaigai amewataka waumini na viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
Amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwasisitiza waumini kuchukua tahadhari za ugonjwa huo na kuhakikisha miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya inazingatiwa.
Ameeleza hayo leo Jumamosi Juni 27, 2021 katika Kanisa la Kilimanajro Revival Temple (TAG) lilipo Moshi Mjini.
"Tuendelee kushirikiana kuliombea Taifa letu hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapita katika janga hili la corona, tuendelee kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya ili tuvuke wote salama."
"Kuvaa barakoa ni muhimu hasa mnapokuwa kwenye msongamano, hakikisheni mnanawa mikono kwa sabuni kwa kutumia maji tiririka na sehemu ambayo hakuna maji tumieni vitakasa mikono," amesema Kagaigai.
Mbali na corona amewataka viongozi wa dini mkoani humo kushirikiana naye kukemea maovu ikiwemo unywaji wa pombe uliopindukia ambao unarudisha nyuma maendeleo ya Taifa na kwa mtu mmoja mmoja.
"Wachungaji pamoja na waumini mliopo hapa, tushirikiane pamoja na kukemea yanayoturudisha nyuma kimaendeleo, kuna vijana sasa hivi wamejiingiza kwenye ulevi, ni jukumu letu sote kushirikiana kukemea haya yote," amesema Kagaigai
Mchungaji wa kanisa hilo, Ron Swai amesema wataendelea kushirikiana na mkuu huyo wa mkoa kuhakikisha yote yanayotakiwa kufanyika yanatimizwa.