RC Katavi aonya upotoshaji sensa ya watu na makazi

Baadhi ya wananchi waloojitokeza kushiriki bonanza la sensa wakivuta kamba ikiwa ni mchezo wa kuhamasisha sensa. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • RC Mwanamvua amewataka wananchi kuwataja watu watakaowabaini wanaopotosha sensa ili wachukuliwe hatua

Katavi. Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ameitaka jamii kuepukana na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu sensa ya watu na makazi.

Akizungumza na hadhara ya wananchi leo Agosti 15, 2022 katika bonanza la kuhamasisha wananchi kushiriki sensa, Mwanamvua amesema wakibaini watu wenye tabia hiyo watoe taarifa kwa viongozi na vyombo vya dola wachukuliwe hatua.

"Tutashughulika nao vizuri kisheria hatutawaacha salama kwasababu watakuwa hawana nia nzuri na rais," amesema.

Aidha amewataka wananchi kutowaficha watu wenye ulemavu, wanatakiwa kuhesabiwa ili watengenezewe utaratibu mzuri wa kupata huduma.

"Kupitia bonanza hili tulilofanya natumia nafasi hii kutangaza kuwa sasa tunao mabalozi wa sensa kupitia makundi yetu maalumu.

"Tunao bodaboda, bajaji, wajasiriamali, machinga na wengine tunawakabidhi kazi hii ya kuhamasisha sensa mkaifanye kupitia mabango na kuzungumza na wateja wenu," amesema,

Naye Ally Hamis ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Mpanda amesema bonanza hilo limeongeza uelewa kuhusu masuala ya sensa kutokana na elimu iliyotolewa.

"Tunaenda kuhamasisha wengine wahesabiwe ili serikali ipate idadi kamili rai yangu watu wajitokeze tarehe 23, tukihesabiwa ni faida yetu sisi," amesema.

Bonanza hilo lilofanyika viwanja vya Azimio Manispaa ya Mpanda limeambatana na matembezi ya hiari, michezo ya mpira wa miguu na kuvuta kamba lengo ni kuhamasisha jamii kushiriki sensa.