RC Kilimanjaro awatuliza wananchi mgogoro wa ardhi
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akimimina zege katika moja ya bikoni iliyowekwa katika eneo la Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kama sehemu ya kutambua mipaka kati ya wananchi wanaouzunnga uwanja wa ndege na KADCO, lengo ikiwa ni kumaliza migogoro ya mipaka ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 20. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Serikali imewataka wananchi wa vijiji vitano vya kata ya Kia, wilayani Hai ambavyo vina mgogoro na Kampuni ya Usimamizi na Uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO) kuwa na utulivu wakati shughuli za tathmini na upimaji ardhi zikiendelea.
Hai. Serikali imewataka wananchi wa vijiji vitano vya Kata ya Kia wilayani Hai ambavyo vina mgogoro na kampuni ya usimamizi na uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO) kuwa na utulivu wakati shughuli za tathmini na upimaji ardhi zikiendelea kwenye eneo lenye kilomita za mraba 110.
Akizungumza wakati wa uzunduzi wa shughuli ya uwekaji bikoni kwenye maeneo hayo leo Novemba 9, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema shughuli hiyo ya upimaji ardhi na tathmini itakapokamilika wananchi ambao watabainika kuingia eneo la Uwanja wa Ndege KIA watalipwa fidia zao za ardhi na mali na kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.
Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 KADCO na wananchi hao wako katika mgogoro wa kugombea ardhi huku wananchi wakidai walimilikishwa na wazazi wao miaka 40 iliyopita na KADCO ikieleza kulimiliki eneo hilo kihalali.
"Leo tumeanza shughuli ya upimaji ardhi na kuweka bikoni kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa KIA na wakati zoezi hili likiendelea tunawaomba wananchi wa maeneo haya kuwa watulivu na hatutaki fujo, tunahitaji amani itawale hapa, wananchi msikubali kushawishiwa na watu ambao sio wakazi wa KIA," amesema RC Babu.
"Nitoe wito kwa wananchi wa Kia na viongozi wa KIA tutekeleze agizo hili la serikali ili tujue ni nani ameingia na ni nani hajaingia eneo la uwanja, Wale watakaobainika wameingia hawataondoka hivi hivi wote watalipwa na kufanyiwa tathmini lakini wanalipwa kwa huruma ya Rais maana eneo hili lina hati ya miaka 99,"amesema RC Babu.
Amewataka wananchi hao kutowachukia viongozi wao waliowachagua kwa kuwa kinachofanyika ni maamuzi ya serikali na ni jambo ambalo lina manufaa kwa wananchi wa wilaya hiyo ya Hai na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Babu amempongeza diwani wa kata hiyo kwa ushirikiano aliouonyesha kwa serikali kushirikiana bega kwa bega na maofisa ambao wanaendelea na shughuli hiyo ya upimaji wa ardhi pamoja na mambo mengine.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wakati maofisa ardhi wanapita katika maeneo hayo ili jambo hilo liweza kufanyika kwa ufanisi.
"Kila mmoja tunaomba atoe ushirikiano hakuna mtu anayemchukia Mtanzania tuone hii kazi ni ya Watanzania wote. Niwaombe viongozi wote mliopo hapa mhakikishe hii kazi mnayofanya ni ya serikali na ni kwa faida ya wananchi hawa inawezakana hawajajua leo lakini baada ya muda watajua na wataona uzuri wa jambo hili," amesema Boisafi.
Diwani wa Kata ya Kia, Tehera Mollel amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuhakikisha wananchi watakaoondolewa kwenye maeneo hayo wanatendewa haki kama serikali ilivyoagiza na kwamba hawawezi kupingana na serikali katika maamuzi iliyochukua.
"Tutashirikiana na mkoa mpaka tumalize hili zoezi ninachoomba mtuangalie kwa jicho la huruma watendewe haki hawa wananchi wetu ambao tayari maeneo yao yameonekana yameingia kwenye eneo la serikali ili wapate haki zao," amesema Mollel.