RC Makongoro awataka ma DC kuwachukulia hatua watendaji wabovu
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, akizungumza baada ya kuwaapisha wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, mjini Babati. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Manyara wameagizwa kuwachukulia hatua watendaji wa vijiji na kata wanaofuja fedha za Serikalini
Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amewataka wakuunwa Wilaya za Mkoa huo kuwachukulia hatua kali watendaji wabovu wa kata na vijijini wanakwamisha maendeleo na wanaofuja fedha.
Makongoro ameyasema hayo leo Jumanne Juni 22 kwenye shughuli ya kuwaapisha wakuu wapya wawili wa wilaya, Mbaraka Batenga wa Kiteto na Janeth Mayanja wa Hanang' na kuwakaribisha wawili wapya Dk Suleiman Serera wa Simanjiro na Sezaria Makota wa Mbulu.
Amesema maofisa watendaji wabovu wa Kata na vijijini wanaofuja fedha wasipochukuliwa hatua watazoroesha maendeleo na kuambukiza udhaifu kwa watendaji wengine.
Amesema watendaji wabovu wa vijiji na kata endapo wasipochukuliwa hatua pindi wakifuja fedha huwaambia wenzao wafanye ubadhirifu kwani hawachukuliwi hatua.
"Msiwaonee aibu watendaji ambao wataonekana kukwamisha ufanisi wa mambo kwani serikali inatoa na kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwarahisishia wananchi kupata huduma hizo," amesema.
Mkuu wa wilaya ya Babati, Jacob Twange ambaye anaendelea na wadhifa huo katika wilaya hiyo ameahidi kutekeleza wajibu wake katika nafasi hiyo na kufuata maelekezo yatakayotolewa na mkuu wa mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera amesema japokuwa wilaya hiyo ni kubwa kijiografia ila atasimamia tunu za Taifa zilizopo ipasavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Sezaria Makota ambaye awali alikuwa mkuu wa wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, amesema alishafanya kazi miaka saba kwenye eneo hilo hivyo anategemea kupata ushirikiano wa kutosha.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga amesema japokuwa yeye ni mgeni kwenye nafasi hiyo, ila atajitahidi kushirikiana na viongozi na wananchi wa eneo hilo katika kufanikisha maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja amesema hiii ni mara yake ya kwanza kushika nafasi hiyo ila atahakikisha anasimamia mapato ya halmashauri ya wilaya hiyo yapande zaidi.