Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Malima atoa maagizo kwa kiwanda cha sukari Mkulazi

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alipotembelea kiwanda Cha Sukari Mkulazi wilayani Kilosa kwa ajili ya kuangalia namna kinavyoendelea na uzalishaji wakati wowote. Lilian Lucas

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RC), Adam Malima ametembelea Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na kutoa maagizo mbalimbali ikiweko kuwataka kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji.

Kilosa. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameuagiza uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi mkoani huyo kutoa elimu kwa wakulima wa zao la miwa ili kuongeza uzalishaji na malighafi ya kutosha kulisha kiwanda hicho.

Malima ametoa agizo hilo leo Jumanne 25, 2023 alipotembelea kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Mbigiri, wilayani Kilosa ambacho kinamilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Jeshi la Magereza.

Malima amesema kiwanda hicho ambacho kitazalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka na kupunguza uagizaji wa shehena za sukari kutoka nje ya nchi pamoja na kuchangia upatikanaji wa ajira kwa Watanzania.

Mkuu huyo wa mkoa, ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wakulima ambao watazalisha miwa itakayokidhi mahitaji ya kiwanda hicho.

“Sasa hawa wakulima wadogo huwa wanaandaliwa na ndivyo tulivyokubaliana, sasa hivi bodi na watu wengine watengeneze mpango wa kuwaandaa wakulima ili waweze kuendana na mahitaji ya kiwanda,” amesema Malima

Malima amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kianze uzalishaji wake.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari, Filbert Mpozi amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 Serikali haiagizi sukari kutoka nje hivyo kiwanda hicho kipya kitatimiza lengo lake kutoagiza Sukari nje ya nchi.

Amesema kiwanda hicho kitaifanya Serikali kutotumia fedha nyingi za kigeni kuagiza sukari nje ya nchi lakini pia kiwanda hicho kitaongeza ajira kwa Watanzania.

Hata hivyo, Filbert ameipongeza Serikali kupitia NSSF kwa uwekezaji huo ambao utasaidia nchi kujitegemea kwenye bidhaa ya sukari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mkulazi Holding Company, Dk Hildelitha Msita kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo amemshukuru Malima kwa ziara yake na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyoyatoa ikiwemo kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.