Dk Nchimbi: Sabasaba isiwe maonyesho tu, iwe injini ya Dira ya Taifa 2050
Muktasari:
- Tangu kuanzishwa kwa maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DiTF) yamezalisha fursa za biashara na uwekezaji zenye thamani ya takribani Sh129.31 trilioni.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba yanapaswa kuendelea kuwa nguzo ya biashara, uwekezaji na ubunifu itakayosaidia kuifikisha Tanzania kwenye malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika hafla ya Sabasaba Gala iliyofanyika usiku wa Julai 6, 2026 iliyoenda sambamba na ugawaji wa tuzo, Dk Nchimbi alisema maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba ni zaidi ya kusherehekea historia ya maonyesho hayo.
Alisema sherehe hizo za dhahabu ni nafasi ya kutafakari mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na kuweka mwelekeo wa miaka 50 ijayo.
Alisema katika kipindi cha nusu karne iliyopita, Sabasaba imepitia mageuzi makubwa na sasa si maonesho ya bidhaa pekee bali ni jukwaa linalowaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji, wabunifu na taasisi mbalimbali za maendeleo huku likifungua masoko ya ndani na nje ya nchi kwa bidhaa za Tanzania.
“Miaka 50 ni fursa adhimu ya kuangalia tulikotoka, tulipo na tunapoelekea, ili kubaini mafanikio tuliyoyapata na fursa zinazotupasa kuzitumia katika siku zijazo,” alisema.
Alisema hatua hiyo inakuja sasa wakati Tanzania imeanza rasmi kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuanzia Julai 1, 2026, ambayo inalenga kujenga taifa lenye utulivu, uchumi shindani, wananchi wenye ujuzi, ubunifu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia.
Alifafanua kuwa kwa msingi huo, maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba yanapaswa kuwa sehemu ya kujadili namna maonesho hayo yatakavyochangia utekelezaji wa dira hiyo na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda huu.
Dk Nchimbi alisema Serikali imejikita katika kujenga uchumi shindani unaochochewa na sekta binafsi kupitia kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa. Alisema mafanikio hayo hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi, wazalishaji, wawekezaji, wafanyabiashara, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo.
“Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujenga mazingira rafiki ya biashara, lakini mafanikio yatapatikana pale sekta binafsi itakapowekeza zaidi, kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa na kutumia fursa za masoko yaliyopo ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa na serikali katika miaka ya karibuni zimeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji jambo ambalo limeongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa na kuifanya nchi kuwa kivutio kikubwa zaidi kwa wawekezaji.
Pamoja na mafanikio hayo bado kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika sekta za uzalishaji, viwanda na biashara ili kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania na kuzifanya ziweze kushindana kimataifa.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wadau wa sekta ya fedha hususan benki na taasisi nyingine za kifedha, kuweka masharti rafiki ya mikopo kwa wafanyabiashara hasa ndogo na za kati ili ziweze kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao.
Alisema upatikanaji wa mitaji nafuu ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa biashara, kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.
“Katika safari ya kuelekea mwaka 2050, Sabasaba inapaswa kuendelea kuimarishwa ili iwe jukwaa kubwa zaidi la biashara Afrika Mashariki na miongoni mwa maonyesho yenye ushawishi mkubwa barani Afrika,” alisema.
Aliwashukuru waandaaji wa maonyesho hayo, washiriki, wawekezaji, wazalishaji, wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi pamoja na washirika wa maendeleo kwa mchango wao ulioifanya Sabasaba kuendelea kukua kwa miaka 50.
“Tuendelee kushirikiana kujenga Sabasaba iliyo kubwa zaidi, yenye ushindani zaidi na yenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TanTrade, Latifa Khamis alisema wataendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa wajasiriamali wa ndani ili kuwawezesha kufikia masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.
Katika kuakisi hilo, tangu kuanzishwa kwake maonyesho hayo yamezalisha fursa za biashara na uwekezaji zenye thamani ya takribani Sh129.31 trilioni.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha mchango mkubwa wa maonesho hayo katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza nafasi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
“TanTrade itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuhakikisha wafanyabiashara na wazalishaji wa ndani wanashiriki kikamilifu katika maonyesho mbalimbali ya biashara na kupata fursa halisi za kutangaza na kuuza bidhaa zao katika masoko ya nje,” amesema.
Aliwataka Watanzania kuitumia Sabasaba kama jukwaa muhimu la kuonesha ubunifu, kujenga chapa za bidhaa na huduma zao pamoja na kupanua wigo wa masoko yao nje ya mipaka ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga alisema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka ya karibuni yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Alisema kila upande umechangia kwa nafasi yake katika kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
“Wafanyabiashara na wawekezaji wameendelea kuwekeza mitaji yao, kuboresha ubora wa bidhaa na kupanua wigo wa masoko, hatua zilizosaidia kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau hao ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kuvutia uwekezaji zaidi na kufungua masoko mapya akisema ushindani wa biashara duniani unahitaji ubunifu, uzalishaji wenye viwango na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto zinazotokana na mabadiliko ya mazingira ya biashara duniani hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha sera na mikakati inayowezesha wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika masoko ya kikanda na kimataifa.