Dk Nchimbi ataka utatuzi malalamiko utolewaji vyeti vya tathimini ya mazingira
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza wakati wa alipotembelea Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika maadhimisho ya miaka 40 ya baraza hilo.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, kama kuna jambo linalotia doa ni miradi mikubwa ya nchi kuchelewesha kwa kisingizio mbalimbali ikiwamo maofisa kujaribu kupata rushwa
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kulifanyia kazi suala la utoaji wa Vyeti vya Tathimini ya Athari ya Mazingira (EIA), akisema ni eneo linalolalamikiwa kwa madai ya rushwa.
Dk Nchimbi amesema kama kuna jambo linalotia doa ni miradi mikubwa ya nchi kuchelewesha kwa kisingizio mbalimbali ikiwamo maofisa kujaribu kupata rushwa.
"Huu ugonjwa wa kuchelewesha mambo muhimu ili kutengeneza mazingira ya rushwa umekuwa tatizo sana katika maeneo mbalimbali," amesema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Alhamisi Julai 2, 2026 katika maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC, ambapo alipata fursa ya kuelezwa na menejimenti ya baraza hilo kuhusu mipango ya miaka mitano ya taasisi hiyo yenye dhamana ya usimamizi na hifadhi ya mazingira.
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akishika zawadi aliokabidhiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) alipotembelea taasisi hiyo katika maadhimisho ya miaka 40 ya baraza hilo. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Sware.
Hata hivyo, Dk Nchimbi amefafanua jitihada za NEMC za kukabiliana changamoto hiyo zinaonekana.
"Tuone rushwa ni jambo baya, kila mmoja moyoni mwake aseme siwezi kuendekeza mambo ya rushwa kwa sababu yanaangusha nchi yangu.
"Hadi sasa menejimenti inafanya kazi nzuri lakini nataka iendelee namna hiyo. Pia, watumishi mjue NEMC inapolalamikiwa, sisi wote mashabiki wa baraza hili tunakosa usingizi popote tulipo," amesema Dk Nchimbi.
Safari ya NEMC kuwa mamlaka
Dk Nchimbi ameiambia menejimenti ya NEMC kuwa suala la baraza hilo kuwa mamlaka inafanyiwa kazi, akiwataka kutokuwa na wasiwasi kuhusu mchakato huo.
"Kama kipindi hiki ndoto ya NEMC kuwa mamlaka kamili haitatimia basi haiwezi kutekelezwa tena kwa sababu tuna Rais (Samia Suluhu Hassan), aliyewahi kuwa Waziri wa Mazingira na Makamu wa Rais," amesema.
"Ajenda ya NEMC kuwa mamlaka ameanza nayo akiwa waziri, sasa msadizi wake ( Dk Nchimbi) ni ofisa wa NEMC aliyepo likizo. Vijana wa sasa wanasema imeisha hiyo, tuombeane uzima,ili ajenda hii ifike mwisho, " ameeleza Dk Nchimbi.
Ahimiza umoja, mshikamano
Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi awapongeza menejimenti na wafanyakazi wote wa NEMC kwa utekelezaji wa majukumu yao, akiwataka kuwa na umoja na ushirikiano kwa masilahi ya nchi.
"Msiruhusu kiongozi wa juu yako akufikirie kwamba unataka yeye asifanikiwe, jitahidi kumuonesha kuwa yeye anataka afanikiwe. Ukifanya hivyo utamfanya ajisikie yupo salama, na wewe utakuwa salama," amesema Dk Nchimbi.
Amehimiza ushirikiano miongoni mwao akisema maisha ya utumishi wa Serikali ni ya muda mfupi, hivyo hakuna sababu ya kujenga chuki na mtu yeyote bali watekeleze majukumu yao kwa umoja, mshikamano na kuacha na vitendo vya fitina kwenye kazi
Shindano la usafi
Mbali na hilo, Dk Nchimbi ameitaka NEMC kuratibu shindano la usafi ikiwamo upandaji miti, usafi wa miji ikiwezekana mara moja kwa mwaka na washindi wa tano bora wanakabidhiwa zawadi hadharani.
"Waliongozwa kwa usafi wanapewa vyeti hadharani na wale waliongozwa uchafu wanapewa vyeti hadharani nadhani kila halmashauri itajitahidi kukwepa cheti cha aina hiyo," amesema Dk Nchimbi.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Sware amesema katika kikao cha ndani baraza hilo liliwasilisha mpango mkakati kwa kipindi cha miaka 2026/ 27 hadi 2031, akisema limejikita kuongeza ufanisi wa usimamizi wa mazingira na ukaguzi na utekekezaji wa sheria.
"Pia, kuchochea uchumi wa kijani na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Tumemweleza mchango wa NEMC kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050," amesema Dk Sware.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC, Mwanasha Tumbo amesema ziara Dk Nchimbi kwenye baraza hilo, ni heshima kuwa ya dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuendelea kuimarisha mazingira nchini.
Tumbo amesema bodi hiyo imeendelea kushirikiana na menejimenti ya NEMC katika utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi, uwazi na weledi kwa manufaa ya Taifa.
"Mipango ya NEMC kwa miaka mitano ijayo ni kuhakikisha baraza linajitegemea, kwa hiyo tunakwenda kupunguza matumizi ya fedha za misaada na zile zinazotoka serikalini, tutakwenda kufanya kazi kwa bidii," amesema.