RC Mara avunja kamati ya CDC, aagiza Polisi kuwakamata viongozi

Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi amevunja Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyoundwa kwaajili ya kupanga na kusimamia matumizi ya fedha kwaajili ya uwajibikaji (CSR) kutoka mgodi wa Barrick North Mara.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi amevunja Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyoundwa kwaajili ya kupanga na kusimamia matumizi ya fedha kwaajili ya uwajibikaji (CSR) kutoka mgodi wa Barrick North Mara.

Pia, Hapi ameliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata viongozi wa kamati hiyo na kuwahoji kuhusu matumizi ya fedha hizo.

Uongozi wa CDC uliundwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri kwaajili ya kusimamia fedha hizo ambapo wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na viongozi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo huku katibu wa kamati akiwa meneja mahusino wa mgodi.

Akizungumza leo Aprili 20, 2022 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa kamati iliyoundwa na ofisi yake kwaajili ya kuchunguza matumizi ya fedha hizo za CSR, Hapi amesema kuwa kamati hiyo haikuwa na mamlaka kisheria kupanga na kusimamia matumizi ya fedha hizo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria fedha za CSR ni fedha za umma hivyo matumizi yake yanapaswa kuzingatia sheria na taratibu za Serikali na si vinginevyo.

"Hii CDC licha ya kuwa na wajumbe zaidi ya 200 lakini hata mwenyekiti wa halmashauri hakuruhusiwa kuhudhuria vikao vyake walikuwa wanakaaa wanapanga mambo wenyewe mbaya zaidi wanapanga utekelezaji wa miradi bila kuwahusisha wataalamu wa sekta husika sasa unajiuliza gharama za miradi hiyo inatokana na makisio gani" amesema

Hapi ameuagiza uongozi wa mgodi huo kumuondoa meneja mahusiano wa mgodi kwa madai ya kwenda kinyume cha taratibu hivyo uongozi wa mkoa haupo tayari kufanya naye kazi.

"Huyu meneja mahusiano hatumtaki muondoeni na kama nyie mna shida naye mpangieni sehemu nyingine sababu mambo yake yako kinyume na utaratibu na ninaomba niishie hapa mimi ni kiongozi nimekula kiapo sio kila kitu nikisema hadharani" amesema

Awali akikabidhi taarifa ya kamati, mwenyekiti wa kamati hiyo, Anselem Daniel amesema kuwa wamebaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa uliifanywa na viongozi wakiwemo wa Serikali katika matumizi ya fedha zilizotolewa na mgodi kati ya mwaka 2018 hadi 2021.

Amesema kuwa kamati hiyo iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Robert Gabriel ikiwa na wajumbe watano inapendekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina dhidi ya viongozi hao ambao hata hivyo majina yao hayakuwekwa hadharani.

Amesema kuwa wamebaini kuwa wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika halmashauri za wilaya ya Tarime Vijijini na Tarime Mji taratibu za manunuzi hazikufuatwa hali iliyoplekea ununuzi wa vifaa vya ujenzi vingi kuliko mahitaji.

"Lakini pia jamii haikuwa ikishirikishwa kwenye uibuaji wa miradi na utekelezaji wake hivyo ipo haja ya mamlaka za kiuchunguzi kufanya uchunguzi wa kina na hatimaye hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika " amesema Daniel