RC Mbeya awaonya ma-DC, ma-DED fedha za Rais

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wa mkoa huo kusimamia vizuri matumzi ya Sh15.83 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19.


Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wa mkoa huo kusimamia vizuri matumzi ya Sh15.83 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Akizungumza na wakuu wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, kamati ya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na machifu leo Alhamisi Oktoba 14,2021, RC Homera amesema fedha hizo zimeingia na zinatakiwa kuanza kufanyiwa manunuzi.

"Ndugu zangu pesa hizo ni za moto, nawaeleza tena zikitumika ndivyo sivyo watu watapoteza vibarua vyao na mimi sitoweza kuvumilia. Rais anawekeza kwenye miradi ya kimkakati halafu watu wachache wakavuruga kwa tamaa zao binafsi sitofumbia macho," amesema.

Aidha Homera ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanza ufuatiliaji wa matumizi wa fedha hizo kuanzia hatua za manunuzi mpaka utekelezaji wa miradi hiyo itakapokamilika kwa muda ambao Serikali imeelekeza.

Kuhu chanjo za Uviko-19 amesema; "Niwaeleze jambo jema, jana Jumatano Oktoba 13, 2021 tumepokea chanjo mpya ya Uviko -19 dozi 41,983 ambazo zitaendelea kutolewa  katika halmashauri zote za mkoa"amesema.