RC Mbeya: Wanawake kopeni kwa miradi mikubwa
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akizungumza na wanawake Wafanyabishara Mkoa wa Mbeya ambao wana tabia kunufaika na mkopo wa Sh 500 milioni kutoka benki ya Azania. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Katika juhudi za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, Sh500 milioni kutolewa mkopo kwa wanawake wafanyabiashara mkoani Mbeya.
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wafanyabishara wanawake mkoani hapa kuchangamkia fursa za mikopo ya zaidi ya Sh 500 inayoanza kutolewa na benki ya Azania.
Homera ametoa kauli hiyo jana June 8,2023 ikiwa ni usiku wa Mwanamke hodari ulioandaliwa na benki hiyo sambamba na kueleza mipango mikakati ya kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo nafuu ili kuchochea biashara na uchumi.
“Wanawake ondoeni shaka fursa ipo wazi kakopeni tayari kuna zaidi ya Sh 500 milioni zitatolewa kama mkopo nafuu, na nimeambia kuwa Azania inalenga kuwafikia wafanyabishara wanawake zaidi ya 400 mkoani hapa,” amesema Homera.
Ameongeza: “Ni matarajio yangu kupitia ninyi mtaongeza wigo wa kuwekeza kwenye mikopo ya ujenzi wa hoteli, nyumba za kisasa kulala wageni ambazo zitavutia wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaoingia kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA),” amesema.
Homera amesema kuwa mikopo kwa wanawake ni fursa pekee kwa mabenki kuongeza wigo wa kuvutia wateja wengi kwa kuzingatia kwa sasa wanawake ndio nguzo ya familia.
“Sio kwamba wanaume hawapo wapo nao kuna fursa zao za kukopa lakini kwa miaka ya sasa idadi kubwa wanasubiri Mama apambane yeye kazi yake kuomba kuvuliwa koti, mkanda na viatu jambo ambalo wengi wanabweteka,” amesema Homera na kuongeza;
“Maonyesho ya nane nane mwaka huu yanafanyika tena kitaifa Mkoa wa Mbeya hivyo ni matarajio ya Serikali kuona mikopo inatolewa na uwekezaji mkubwa ukifanywa ili jiji liendane na hadhi ya uwepo wa miradi mikubwa ya barabara njia nne, uwanja wa SIA.”
Meneja wa Benki hiyo Saimon Mahimbi amesema wameboresha mifumo ya utoaji wa mikopo kwa wanawake kutoka wastani wa Sh200, 000 mpaka 500 million sambamba na kuondoa makato mbalimbali.
Amesema wanatambua mchango mkubwa wa wanawake katika kuchangia pato la taifa hivyo kama benki wataendelea kutoa mikopo pasipo kuwaacha wafanyabishara wadogo wenye mitaji midogo kuinuka kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mbeya Edna Mwaigomole amesema uwepo wa mikopo ni fursa kubwa kwa wanawake mkoani Mbeya, ni wakati sasa wa kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati kupitia akaunti ya Mwanamke hodari.