RC Mghwira awaita wadau kununua mahindi yaliyozuiwa Kenya
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amewataka wadau mbalimbali kujitokea kununua mahindi yaliyozuiwa kuingia nchini Kenya yakidaiwa kuwa na sumu kuvu jambo ambalo si kweli.
Rombo. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amewataka wadau mbalimbali kujitokea kununua mahindi yaliyozuiwa kuingia nchini Kenya yakidaiwa kuwa na sumu kuvu jambo ambalo si kweli.
Amesema tani 432 za mahindi hayo ni salama na yamethibitishwa na watalaam.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili mosi, 2021 katika mpaka wa Holili mkoani Kilimanjaro baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya ulinzi na usalama.
"Niwatoe hofu Watanzania na walimwengu wote popote pale walipo..., napenda kuwaeleza kuwa mahindi yetu ni salama na yamethibitishwa na wataalamu wetu.”
"Nawaomba wanunuzi na wachuuzi wengine mahali walipo kwamba mahindi yapo ya kutosha, kama kuna taasisi au mtu binafsi anahitaji mahindi afike ofisini kwangu au kwa mkuu wa Wilaya ya Rombo tutawapa maelekezo mahindi yalipo ili waweze kununua," amesema Mghwira.