RC Mtaka azuia Sh47 milioni ziara ya madiwani

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akizungumza kwenye kikao cha utendaji kazi na watumishi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma leo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amekataa kuidhinisha ombi la Sh47 milioni kwa ajili ya ziara ya Madiwani wa jiji hilo, akidai kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amezuia ombi la Sh47 milioni zilizokuwa zitumike kwenye ziara ya Baraza la madiwani na watumishi zaidi ya 60 akisema ni matumizi mabaya ya fedha.

Mtaka aliisoma barua ya maombi hayo leo Jumatano  Oktoba 20 iliyokuwa na kichwa cha habari; “Maombi ya kibali cha kufanya ziara ya mafunzo kwa waheshimiwa madiwani na tawala kwa halmashauri za jiji la Dodoma katika jiji la Mbeya na Arusha,” kwa watumishi 1,500 waliohudhuria katika mkutano uliolenga utumishi na utawala bora jijini hapa.

Kwa mujibu wa barua hiyo, madiwani hao walitaka kujifunza elimu ya ukusanyaji mapato, usafi wa mazingira, uanzishwaji na uendeshaji wa shule za michepuo ya kiingereza, uwekezaji wa mfuko wa elimu, utawala bora, usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na utatuzi wa migogoro na changamoto zake.

“Wakati vyombo vya habari vinaonesha wenzetu walivyotekeleza malengo ya Mheshimiwa Rais, eti huko Mbeya waandishi wanaripoti ziara ya madiwani kujifunza uendeshaji wa shule za International.

“Kwa nini tutumie Sh47 milioni kwenda kujifunza namna ya kuendesha za English medium school, Serious?  na ukusanyaji wa mapato eti na kutunza mazingira, Rais atatufukuza kazi sisi wote na ataniuliza niko serious kweli ” amehoji RC Mtaka.

Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akizungumzia kuhusu uwepo wa malalamiko ya wananchi kuhusu huduma mbovu kwenye ofisi ya jiji amesema bado kuna changamoto hasa kwenye idara ya ardhi.

Akichangia kero yake kwenye mkutano huo mtumishi kutoka masjala ya afya, Catherine Mwombeki amesema watumishi wanapata changamoto kutoka kwa viongozi wao kwa kuwageuza watumishi wa ndani kinyume na maadili.

“Utakuta unamhudumia mwananchi na bosi wako anakwambia njoo ukaninunulie chapati, sasa unajiuliza kwenda kumnunulia chapati na kumhudumia mteja kipi bora? Ukichelewa kidogo anaanza kukugombeza hii watumishi inatuumiza sana,” amesema.