RC Mwanza apiga marufuku mikusanyiko kukabili corona

RC Mwanza apiga marufuku mikusanyiko kukabili corona

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amepiga marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima kama njia ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amepiga marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima kama njia ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumanne Julai 20, mkuu huyo wa mkoa amesema uamuzi huo unatokana na ukweli kwamba Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa nchini yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

“Mkoa wetu, hasa jiji la Mwanza ni Hub (kitovu) cha mikusanyiko ya watu kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na nchini jirani ambako kuna kasi kubwa ya maambukizi ya corona,”amesema Gabriel.

Huku akionyesha msisitizo, kiongozi huyo amesema; “Viongozi lazima kufanya kila linalowezekana kulinda watu; ni bahati mbaya wengi bado hawazingatii kanuni za afya za kujikinga kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa majitiririka, kutakasa mikono kwa kwa kutumia vipukusi na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,”

Gabriel ameviomba vyombo vya habari kusaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu kanuni za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona kunusuru maisha ya watu.

“Hatuwezi kukataza watu kwenda sokoni na kwenye shughuli zingine za kiuchumi zinazokusanya wengi; tunachosisitiza ni kwamba kila anayeenda kwenye kusanyiko azingatie kanuni ya kujilinda na kuwalinda wengine; vyombo vua habari saidieni katika eneo hilo,” amesema Gabriel

Akijibu swali iwapo amri yake imelenga kukwamisha kongamano la Katiba mpya lililoitishwa kesho Julai 21 na Chama cha Demakrasia na Maendeleo (Chadema), mkuu huyo wa mkoa amesema; “Watu wanaweza kuwa na tafsiri na hisia tofauti, lakini kwa hakika amri yangu haijamlenga mtu, kikundi wala taasisi yoyote.”

Amesema iwapo kuna watu wana sherehe au jambo lao wanaloamini ni lazima lifanyike kwa kukusanya watu, basi wahakikishe wanapata vibali kutokana mamlaka zinazohusika na kuzingatia kanuni za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona kwa mujibu wa maelekezo ya wataalam wa afya.

"Mwenye sherehe au shughuli yake anayodhani lazima ifanyike na kukusanya watu wengi lazima azingatie kanuni ya kujikinga dhidi ya corona baada ya kupata vibali kutoka mamlaka husika," amesema Gabriel

Akizungumzia amri hiyo, Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Zakaria Obadi amesema, “Sisi tunaendelea na maandalizi ya kongamano letu litakalofanyika kwa kuzingatia kanuni zote za kujikinga dhidi ya virusi vya corona. Chadema ni champions katika eneo hilo la kuzingatia kanuni za afya za kujikinga dhidi ya corona,”

Obadi amesema chama hicho kimepokea kwa tahadhari kubwa tamko la amri ya mkuu wa mkoa na uongozi wa juu utalizungumzia wakati wowote.