RC Njombe aonya wananchi kuiba vifaa vya ujenzi wa barabara

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya amewaonya wananchi mkoani Njombe kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya wizi wa vifaa mbalimbali ambavyo vinatumika katika ujenzi wa barabara mkoani Njombe.

  

Njombe. Mkuu wa mkoa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya amewaonya wananchi mkoani Njombe kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya wizi wa vifaa mbalimbali ambavyo vinatumika katika ujenzi wa barabara mkoani humo.

Onyo hilo amelitoa leo Alhamisi 25 Novemba 2021 wakati wa uzinduzi wa kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo.

Amesema mafanikio ya miradi hiyo ya ujenzi wa barabara mkoani hapa itategemea ushirikiano mkubwa kati ya wakandarasi na wananchi kwenye meneo mbalimbali.

Amewataka madiwani na wenyeviti wa halmashauri mkoani hapo kuwahimiza wananchi kwenye maeneo yao kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.

"Hatutarajii wananchi wetu kujihusisha na wizi ama ununuzi wa vifaa vya ujenzi kama Nondo na Saruji" amesema Rubirya.

Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuilinda miradi hiyo kwani pindi itakapokamilika wanufaika wakubwa watakuwa wananchi wenyewe.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Njombe,  Ruth Shalluah amesema miradi mingi imekamilika katika  utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita.

Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22  jumla ya Sh17 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika mkoa wa Njombe.