RC Tabora aamuru mganga hospitali ya Kaliua akamatwe

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Tabora (RC), Dk Batilda Burian ameamuru Jeshi la Polisi kukamatwa na kuwekwa ndani mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, Irene Apina kwa tuhuma za kukataa kumhudumia mtoto ambaye inadaiwa alifariki baada ya kukosa matibabu.

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora (RC), Dk Batilda Burian ameamuru Jeshi la Polisi kukamatwa na kuwekwa ndani mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, Irene Apina kwa tuhuma za kukataa kumhudumia mtoto ambaye inadaiwa alifariki baada ya kukosa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 28, 2021 RC Burian amesema amefikia uamuzi huo baada ya mganga huyo kusimamishwa kazi na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua (DC), Paul Chacha kutokana na tuhuma hizo.

Juzi wakati DC Chacha akizungumza na watumishi wa afya alimsimamisha kazi Apina baada ya kupata taarifa kuwa alikataa kumhudumia mtoto wa miaka mitano na baadaye mtoto huyo kufariki dunia kwa kukosa matibabu.

RC Burian amesema kuwa hatua alizochukua Mkuu wa Wilaya za kumsimamisha kazi ni ndogo hivyo akaagiza mganga huyo akamatwe na kuwekwa ndani ili aone uchungu wa mtu kufiwa na mtoto wake.

"Serikali hauwezi kuvumilia watumishi wenye roho za kishetani kama mganga huyo" amesema

Naya Mkuu wa Wilaya ya Kaliua (DC), Paul Chacha amesema tukio hilo limemkasirisha hivyo imemlazimu kumsimamisha kazi mganga huyo.

DC Chacha amesema kuwa wakati wa kikao cha watumishi wa afya alimuuliza mganga huyo kama alivyofanya ni vizuri, akisema alijibu hapana huku akilia.

Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Dk Lusubilo Adam amewataka watumishi wa Afya kufanya kazi zao kwa weledi kwa vile wanategemewa na jamii katika utoaji wa huduma.