RC Tanga: Marufuku kuomba uhamisho kisingizio hali ya hewa

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima 

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima  amepiga marufuku watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuomba uhamisho kwa kusingizia hali ya hewa kuwa inawaathiri kiafya. 


  

Lushoto. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amepiga marufuku watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuomba uhamisho kwa kusingizia hali ya hewa kuwa inawaathiri kiafya.

Ametoa agizo hilo leo Jumamosi Novemba 27, 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi  ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha za tozo na zile za Uviko zilizotolewa na Serikali.

Malima amesema kuhama kwa watumishi wakiwamo walimu imeathiri wilaya hiyo na hasa kushuka kiwango cha elimu.

" Nasikitika ninapoona kuna mafaili mengi ya watumishi wa umma kutaka kuhama kwa kisingizio cha baridi kali. Katibu Tawala acha kupokea maombi hayo mara moja, nataka kupata takwimu za uwiano walimu wa maeneo ya milimani na wale mjini" amesema Malima

Amesema katika wilaya za Mkoa wa Tanga zote ni Lushoto pekee iliyoko nyuma kielimu licha ya kuwa na historia ya kuwa na wasomi wengi na kwamba juhudi za pamoja zinatakiwa kuhakikisha kiwango cha elimu kinarejea wilayani humo.

" Kuna shule Lushoto zina walimu watatu wakati sehemu zingine walimu wapo hadi 25 habari hiyo sitaki kuisikia. Watoto wa Lushoto wana haki ya kupata haki ya elimu kama iliyo kwa wengine. Somesheni watoto wenu ili wapate elimu kesho wawe madaktari na kada zingine za kitaaluma.

Ametumia fursa hiyo  kuwataka viongzi wa Serikali za wilayani humo kuhimiza watoto kupelekwa shule nakwamba hataki kusikia watoto wanaolewa wakiwa na umri mdogo.

Kuhusu miradi hiyo  ya Vituo vya afya na Madarasa amesema ni lazima wahakikishe wanamaliza mapema ili waweze kupata fedha zingine na wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza waweze kupata madarasa bila vikwazo .