REA kusambaza mabomba ya gesi Pwani na Lindi

Mkurugenzi Mkuu wa wakal wa nishati vijijini (REA), Hassan Saidy akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro juu ya mradi wa Ujenzi wa kituo Cha kupooza na kusambaza umeme Cha Ifakara. Picha na Lilian Lucas.

Muktasari:

  • Mradi huo wa majaribio unatarajia kuanza mwakani katika vijiji vya mikoa hiyo ya Pwani na Lindi utatekelezwa kwa pamoja kati ya REA na shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) kwa gharama ya Sh6 bilioni.

Morogoro. Wakala wa Nishati Vijiji (REA) inakusudia kusambaza mifumo ya mabomba ya gesi asilia kwa wananchi wa mikoa ya Pwani na Lindi ili kuwawezesha wananchi kupata nishati mbadala wa kuni na mkaa.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo leo Desemba 8, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya utekelezaji wa miradi ya kusamba nishati vijijini katika ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Ifakara wilayani Kilombero Mkoani Morogoro.

Mradi huo wa majaribio unatarajia kuanza mwakani katika vijiji vya mikoa hiyo ya Pwani na Lindi utafanywa kwa pamoja kati ya REA na shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) ambao ndio watasambaza mabomba ya gesi hiyo asilia.

Mhandisi Saidy, amesema wao kama REA wameufadhili mradi huo zaidi ya Sh6 bilioni kwa TPDC kuutekeleza.

Mkurugenzi huyo wa REA amesema kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pia wamelenga kusambaza majiko banifu 200, 000 na kuwajengea mitambo ya kuzalisha Bio- Gas katika taasisi za Umma zinazohudumia kuanzia watu 300 hapa nchini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus, amesema mradi wa REA katika ukanda wa Morogoro utasaidia kuhamasisha thamani ya kilimo katika ukanda wa kilimo mikoa ya Kusini mwa Tanzania ikiwemo Morogoro.