Rea yatumia Sh189 bilioni kuiangaza Mtwara

Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi, Jones Olotu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akitoa taarifa ya mkoa wa Mtwara kuhusu usambazaji wa umeme vijijini mbele Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (Aliyekaa mbele) katika ofisi za TANESCO Mtwara.
 

Muktasari:

  • Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) mkoani Mtwara, imetumia Sh189 bilioni kukamilisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya kusambaza nishati ya umeme, na hivyo kuchochea mapinduzi ya kijamii na kiuchumi.

Dodoma. Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) mkoani Mtwara, imetumia Sh189 bilioni kukamilisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya kusambaza nishati ya umeme, na hivyo kuchochea mapinduzi ya kijamii na kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Septemba 15, 2023 na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini Jones Olotu wakati akizungumza katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayoendelea mkoani hapa.

Olotu amesema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo ikiwemo miradi ya Rea mzunguko wa pili, mradi wa kusambaza umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo.

Pia zimetumika katika mradi wa kusambaza umeme kwenye vituo vya afya na visima vya maji ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ukiwemo Uviko-19 na mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji awamu ya tatu (Peri Urban III).

Aidha Olotu amesema Mkoa wa Mtwara una vijiji 785, ambapo hadi kufikia Septemba 10, 2023; jumla ya vijiji 540 vimeunganishwa na umeme kupitia miradi mbalimbali na kwamba vijiji 345 vitapatiwa umeme kupitia mradi wa Rea awamu ya tatu, mzunguko wa pili, unaoendelea kutekelezwa.

Ili kuongeza kasi na kufikia lengo la Serikali la kufikisha umeme katika vijiji vyote, Olotu amesema wakala uliongeza kazi kwa Makandarasi katika vijiji 112 ambavyo havikuwa vimejumuishwa katika mpango wa awali na hivyo kufikia jumla ya vijiji 276 katika wigo wa kazi.

“Kutokana na uhitaji mkubwa wa kuwafikia wateja wengi zaidi, Wakala uliongeza kilomita 2 za umeme wa msongo mdogo kwa wateja 42 kila kijiji na kufanya kuwa na jumla ya vijiji 276 vijivyopo katika fungu (Lot 20) la mradi wa Rea III, mzunguko wa pili,” amesema Olotu.