Rihanna, LVMH wachemsha mambo ya fasheni

Friday February 12 2021
Rihanna pic

Mwanamuziki nyota wa Marekani, Rihanna, ambaye tangu mwaka 2016 hajatoa nyimbo zozote, ameamua kufunga kampuni yake ya mitindo ya mavazi ya Fenty kwa makubaliano na kampuni mshirika ya LVMH, ambayo inatengeneza bidhaa za kifahari.

Kampuni hiyo imefanya kazi chini ya miaka miwili.

Makubaliano ya kufunga shughuli za mavazi hayataathiri uzalishaji wa nguo za ndani unaofanywa na Savage X, kama ilivyo kwa kampuni ya vipodozi ya Fenty Beauty na Fenty Skin.

LVMH ilisema kuwa shughuli za uzalishaji nguo za mtunguo (ready-to-wear) za Fenty zitasimamishwa kwa muda kusubiri hali kuwa nzuri.

Wachambuzi wa fasheni wanasema ingawa Rihanna ana wigo mkubwa wa mashabiki, bei za nguo za chapa za Fenty zilikuwa juu kiasi kwamba wengi walikuwa hawawezi kuzimudu, yahoo.com imeandika.

Lakini pande hizo mbili, LVMH na Rihanna, zimeahidi kujikita katika maendeleo ya muda mrefu ya kufanya kazi pamoja au "Fenty ecosystem".

Advertisement

Rihanna, ambaye jina lake halisi ni Robyn Rihanna Fenty, alikuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuongoza kampuni ya mavazi chini ya chapa ya LVMH wakati Fenty ilipozinduliwa mwaka 2019.

Lakini kumekuwa hakuna kitu chochote kilichotumwa katika akaunti ya Instagram ya chama hiyo tangu kuanza kwa mwaka huuna hakuna mitindo mipya iliyotolewa tangu Novemba mwaka jana.

Kujiingiza kwa Rihanna katika ulimwengu wa mitindo kuliathiri shughuli zake za muziki.

Akiwa anajulikana kwa kutoa albamu moja kwa mwaka, nyota huyo wa muziki hajatoa nyimbo tangu mwaka 2016.

Advertisement