RIPOTI: Kasi ndogo barabarani inachangia umasikini

Muktasari:

Usafiri unakukwamishaje kujikwamua kiuchumi? Unadhani kama kasi yako ya kufika sokoni ingeongezeka uchumi wako ungeimarika zaidi ya ulivyo sasa?

Usafiri unakukwamishaje kujikwamua kiuchumi? Unadhani kama kasi yako ya kufika sokoni ingeongezeka uchumi wako ungeimarika zaidi ya ulivyo sasa?

Wataalamu wa masuala ya uchumi na fedha wanasema barabara ni kati ya nyenzo muhimu za kupunguza umasikini na kuongeze kipato cha mwananchi kuanzia wa shambani anayelima mazao mpaka wa kiwandani zinakozalishwa bidhaa.

Ripoti iliyochapishwa na Shirika la fedha Duniani (IMF) mwezi uliopita inaonyesha ubora wa barabara ni kati ya vitu vyenye mchango mkubwa kwenye kipato cha mtu mmojammoja hata uchumi wa Taifa.

Ripoti hiyo inayoitwa ‘Where are the world’s fastest roads?’ inasema barabara zinazoruhusu magari kutembea kwa kasi kubwa huwezesha abiria na bidhaa kufika masoko ya mbali haraka hivyo kuongeza tija, kupunguza umasikini na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na uchumi.

Utafiti huo uliohusisha barabara za mataifa 162 duniani kote ukiwezeshwa na teknolojia ya Google Maps, uliangalia wastani wa muda unaotumika kusafiri umbali wa walau kilomita 80 kutoka kwenye mji mkubwa.

“Matokeo ya utafiti wetu yanaonyesha ubora wa barabara una uhusiano mkubwa na muda unaotumika kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Utafiti huo ulioongozwa na Dk Mauricio Soto, naibu mkuu wa idara ya sera za matumizi ya IMF akishirikiana na Mariano Moszoro, mchumi mwandamizi wa shirika hilo unasema kasi inayoruhusiwa ni miongoni mwa vigezo muhimu vya kupima ubora wa barabara.

Utafiti huo unaonyesha barabara zenye kasi kubwa zaidi zinapatikana kwenye mataifa yaliyoendelea ikiwamo Marekani, Ureno, Saudi Arabia na Canada, huku nchi masikini, ikiwamo Tanzania, zikiwa na kasi ndogo zaidi. Kwa Afrika, ni nchi nne pekee zina barabara bora zinazoruhusu kasi kubwa ambazo ni Morocco, Afrika Kusini, Namibia na Botswana.

Kwenye mataifa yaliyoendelea, utafiti umebaini barabara zinaruhusu gari kutembea kwa kasi ya wastani wa kilomita 107 kwa saa wakati kwenye nchi masikini ni kilomita 38 kwa saa.

“Wastani wa mwendo wa gari ni kipimo imara kinachodhihirisha ubora wa barabara zilizopo,” inasema ripoti hiyo.

Kasi, ripoti inafafanua kuwa ni kigezo rahisi kinachoweza kutumiwa na watunga sera pamoja na watu wa mipango kutathmini uwekezaji wanaoufanya kujenga barabara kwa kulinganisha na hali ilivyo kwa majirani zao.

Tathmini hiyo, wanasema inaweza kutumika pia kuboresha kasi ya barabara ndogo ambazo ni muhimu katika baadhi ya maeneo. Utaratibu huo, ripoti inasema utazisaidia nchi zinazoendelea kuondoa vikwazo vilivyopo barabarani, hivyo kuongeza ushindani wao katika kusafirisha bidhaa na abiria.

Hata hivyo, utafiti huo unasema tathmini ya kasi iliyofanywa haijahusisha usalama barabarani, uwepo wa namna nyingine za usafiri mfano reli na meli, wala msongamano. Hata changamoto za uhandisi wa ujenzi wake nazo hazijazingatiwa pia.


Umasikini

Katika muongo uliopita, Tanzania ilishuhudia ukuaji mzuri wa uchumi kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka uliosaidia kupambana na umasikini ambao bado ni tatizo.

Baada ya utekelezaji wa mikakati mingi ya Serikali kati ya mwaka 2001 hadi 2007, taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ijulikanayo kama ‘Tanzania Mainland Poverty Assessment Reoprt’ ya mwaka 2020 inasema wastani wa umasikini ulishuka mpaka asilimia 26.4 kutoka asilimia 34.4 mwaka 2018.

Kutokana na ongezeko kubwa la watu, kasi ya ukuaji uchumi haikupunguza idadi ya mafukara nchini, kwani mwaka 2018 walikuwapo milioni 14 waliokuwa wanaingiza chini ya Sh49,320 kwa mwezi kwa viwango vya kitaifa na milioni 26 wanaopata dola 1.9 ya Marekani sawa na Sh4,370 kwa siku ya viwango vya kimataifa.

Takwimu zinaonyesha kuna idadi kubwa ya masikini kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na ile ya kanda ya magharibi, sababu kubwa ikielezwa kuwa ni ukuaji mdogo wa sekta zinazoajiri watu wengi, hasa kilimo, uvuvi na mifugo tofauti na wanaopatikana mikoa ya mashariki kwenye sekta za viwanda, huduma na usafirishaji zinazokua zaidi.

NBS inasema umasikini nchini unachangiwa na ujinga wa wananchi na ukosefu wa fursa za kiuchumi kwenye maeneo yao.

“Umasikini na elimu ndogo ya wazazi unawaathiri hata watoto kuajiriwa kwenye nafasi zinazolipa vizuri, hivyo kuchelewesha mabadiliko yao ya kiuchumi hivyo wengi kuendelea kuishi kwenye ufukara,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.


Maoni ya wadau

Kwenye ripoti ya IMF, Tanzania imewekwa kwenye kundi la nchi ambazo magari yanatembea kwa kasi ya kati ya kilomita 30 mpaka 60 kwa saa ambayo ni ya chini zaidi duniani.

Spidi hiyo ndogo inaelezwa kuwa inawachelewesha watu kufika waendako pamoja na bidhaa zinazohitajika. Watu wakichelewa, uzalishaji mali unasimama hivyo kudumaza uchumi. Mali na malighafi nazo zikichelewa kuwasili zinakohitajika, matumizi hayafanyiki wala uzalishaji hauendi kwa wakati.

Damiani Mwakyambiki, mdau wa usafirishaji anasema kuna masharti mengi barabarani yanayomzuia dereva kutembea kwa kujiachia nchini yanayolenga kudhibiti ajali, ingawa bado jinamizi hilo linaiandama Tanzania na kuiweka kati ya mataifa yenye ajali nyingi kwa mwaka.

“Spidi ndogo haijasaidia kupunguza ajali nchini, lakini kila ikitokea ajali sababu inayotajwa ni mwendo kasi. Farasi zamani walikuwa wanakimbia kasi kubwa zaidi ya kilomita 50 kwa sasa iliyopo sasa hivi nchini,” anasema Mwakyambiki.

Utaratibu wa mabasi ya mikoani kulazimishwa kuingia stendi ya kila wilaya bila sababu za msingi, anasema ni kitu kingine kinachofanya safari nchini kutumia muda mwingi.

“Kwenye hizo stendi kuna ushuru wa kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000. Kama kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha kuna wilaya 10 kwa mfano, basi litalazimika kusimama kwa kati ya dakika sita mpaka 10 katika kila stendi hivyo kupoteza kati ya dakika 60 mpaka 70 ambazo zingeweka kuwawahisha abiria wanaosafiri,” anakumbusha.

Ukiacha kuingia stendi, kuna suala la mizani pia ambako kila basi na lori la mizigo ni lazima lipite kupimwa uzito na mpaka safari ikamilike, si chini ya dakika 40 zinakuwa zimetumika kwa ajili hiyo pekee.

“Matokeo yake safari ya kilometa 600 ambayo kiuhalisia ni fupi sana, inachukua hadi saa 10 kukamilika. Katika nchi nyingine huo muda wanakuwa wametengeneza bidhaa kutumia hata mwezi mzima kama sio mwaka,” anasema Makyambiki.

Kutokana na kasi ndogo ya magari barabarani, wadau wanasema ndio unaozifanya kampuni kubwa kutumia zaidi ndege ili kuwahisha mambo yao.

“Ukiangalia kampuni kubwa za madini kama vile GGM au Barick, wafanyakazi wao wanatumia zaidi ndege. Mtu anaweza kulala Dar es Salaam lakini asubuhi akaenda mgodini Mara na jioni akarudi kulala Dar es Salaam. Kwa gari unahitaji siku mbili kwenda Mkoa wa Mara. Utatumia siku nne kwenda na kurudi, huu muda unatosha kuzalisha,” anasema Hilda Gowele, mfanyabiashara wa samaki.

Iwapo barabara zingekuwa rafiki, anasema ingewezekana mtu kutoka Dar es Salaam au Dodoma kufuata sato Mwanza au Bukoba na kurudi nao siku hiyohiyo lakini hilo haliwezekani “labda utumie ndege ambayo gharama zake ni kubwa,” anasema.

Kuhusu uwezekano wa kupunguza ajali barabarani, Mwenyekiti wa kampuni ya Superdoll, Ally Seif Ally anasema iwapo dereva atazingatia ufungaji sahihi wa tairi, zitapungua kwa kiasi kikubwa.

“Watu wengi hawajui utofauti wa tairi la mbele, nyuma au linalofaa kufungwa kwenye trela, mabasi au malori. Tunashirikiana na wadau tofauti wakiwamo trafiki na waongoza watalii kutoa elimu kwani hili likizingatiwa, ajali zitapungua barabarani,” anasema Seif.

Superdoll ambayo mwaka huu imetimiza miaka 30 ya kushirikiana na kampuni ya matairi ya Michelin yenye makao makuu yake nchini Ufaransa, imeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia, kwani hivi sasa inatumia matairi yasiyo na tyubu kwa zaidi ya asilimia 90 wakati nchi nyingine wana asilimia 25 mpaka 30.