Ripoti Maalum: Kituo cha mwendokasi Mbagala chageuzwa danguro, Polisi watajwa

Kituo cha mwendokasi Mbagala Rangi Tatu ambacho bado hakijaisha

Dar es Salaam. Kama ulidhani kutokukamilika kwa mradi wa mwendokasi awamu ya pili kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu kunawakera wakazi wanaohangaika na usafiri kila linapokucha au kukuchwa unajidanganya. Ipo adha nyingine ya vituo vyake kugeuzwa madanguro, walalamikiwa wakubwa wakiwa baadhi ya askari polisi wanaodaiwa ‘kutengeneza fedha’ kupitia biashara hiyo ya ngono.

Ijapokuwa polisi na viongozi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) wanasema hawana taarifa ya kinachoendelea katika vituo vya mabasi hayo, Mwananchi Digital imefanya utafiti na kujiridhisha kwamba biashara hiyo imeshamiri na inafahamika miongoni mwa wakazi wa maeneo husika wakiwamo viongozi wa serikali za mitaa.

“Hayo ni madai. Ndio nayasikia kwako kwa mara ya kwanza, lazima nichunguze nitakupa majibu. Kwa maelezo hayo, binafsi umenipa kazi nifuatilie,”alisema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Sio Kamanda Muliro tu, Ofisa Habari wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) inayosimamia miundombinu hiyo, William Gatambi alisema hana taarifa kuhusu kinachoendelea katika vituo hivyo.

“Katika eneo hilo ipo kampuni ya ulinzi. Kama kuna vitendo vyovyote vya kulala au kufanya tabia hizo sio sahihi na hatuna taarifa, ila nitauliza kuhusu jambo hilo kwa wahusika wa ulinzi,”alisema na kusisitiza, “wakati kituo kipo katika hatua ile (hakijakamilika) hairuhusiwi hata kuingia ndani, hata sisi wenyewe tunapita nje. Hauwezi kuwa utaratibu wa kampuni.”

Wakati Polisi na Dart wakitoa maelezo hayo, katika kituo cha mabasi hayo Mbagala Rangi Tatu biashara hiyo inaelezwa kushamiri na wanaoifanya wanasema wanalazimika kutoa fedha kwa waliopewa dhamana ya kulinda raia na mali zao, “kabla hujatoka gheto (nyumbani) kuja hapa barabarani (Mbagala Rangi Tatu) lazima niwe na Sh10,000 ya kuwapooza watu wa doria ili ukikamatwa usifikishwe kituoni,” anasema Fatuma Hamis (27) (Si jina halisi) mkazi wa Mbagala Rangi Tatu ambaye anajiuza.

Ripoti Maalum: Kituo cha mwendokasi Mbagala chageuzwa danguro, Polisi watajwa

Maelezo ya Fatuma yanashabihiana na ya Grace John (pia si jina halisi) ambaye pia ni ‘dada poa’ katika eneo hilo ambaye awali alisita kueleza namna askari wa doria eneo hilo wanavyowaachia baada ya kuwapa fedha kwa kuogopa endapo habari hii ikichapishwa akisema huenda wasipate tena fursa hiyo.

“Naogopa kusema, nikikuambia tutakuwa hatuachiwi tena. Au lengo lako tulale ndani? (rumande),”anauliza Grace.

Lakini baadaye alikubali kueleza kwa masharti ya kutotajwa jina wala picha zake kuchapishwa mahali popote.

“Pale inategemea, magari ya doria yanapita kuanzia saa nne usiku hadi saa tano usiku hayo hayakamati watu, lakini yapo matatu yanapita kuanzia saa sita hadi saa saba usiku hayo ndiyo yanakuwa na askari wenye sare na wasio na sare (anawaita sungusungu). Hao ndio hukamata,”anasema.

Grace anasema askari wasio na sare huwakamata na kuwapandisha katika gari kisha kuwachukulia fedha na kisha kuwaacha waendelee na biashara yao.

“Wale ambao hawana sare za polisi ndio wanatukimbiza hadi wanatukamata, ukipandishwa katika gari lao hawakufikishi kituoni wana chimbo (eneo la maficho) ambalo mnawapa fedha ili wawaachie muendelee na biashara zenu,” anasema.

Eneo lilivyo na Serikali za Mitaa zaeleza

Eneo hilo linalolalamikiwa kukithiri kwa vitendo hivyo lipo mpakani mwa mitaa miwili, upande mmoja wa kituo hicho kilichopo barabarani kinapakana na Mtaa wa Mbagala Rangi Tatu ambapo mwenyekiti wake, Hafidhi Chaukulu anaeleza kuwa biashara hiyo imeshitadi huku akiwataja polisi.

“Kuna malalamiko polisi wanawaachia (wanaojiuza) sisi tukiwakamata. Hii imepelekea hata walinzi wetu (polisi jamii) wanakuwa sio waaminifu kwa hiyo wakiwakamata wanachukua fedha wanawaachia,” anasema na kuongeza; “changamoto ni kwamba mimi kama mwenyekiti sina mahabusu ya kuwaweka kwa hiyo ukiona kwamba kila ukiwakamata wanarudi unajiuliza kwa nini uendelee kukamata kama wanaachiwa?”

Chaukulu anasema anaongeza, “askari wangu (polisi jamii) waliwahi kupigwa wakiwa wanatekeleza majukumu yao kutokana na tuhuma za kuchukua fedha kwa dada poa.”

Mwenyekiti huyo anaamini kwamba njia pekee ni wanaume kuacha kuifuata huduma hiyo.

Pia anasema ana kikundi cha ulinzi shirikishi ambacho kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa inayozunguka eneo hilo ikiwamo (Mbagala Rangi Tatu, Kurasini Mji Mpya, Mianzini na Mchikichini) wanapambana kuitokomeza tabia hiyo.

Kwa upande mwingine kituo hicho cha mwendokasi kimepakana na Mtaa wa Mchikichini na kaimu mwenyekiti na mjumbe wa mtaa huo, Faraji Kimboko anasema tayari wamefanya oparesheni za kuwaondoa.

Wananchi walalamika

Sio kila mtu anaifurahia biashara hiyo, mfanyabiashara wa viatu katika eneo la kituo hicho cha Mbagala Joshua Mzinga anasema haiwapendezi na wanashangaa kuona wakikamatwa na polisi wanarudi.

“Tunapata shida sana hapa wafanyabiashara, asubuhi tukifika tunakuta mabaki ya kondomu zilizotumika katika maeneo yetu ya biashara. Tunashangaa likija gari la polisi wanakamatwa lakini baadaye wanarudi tena kama kawaida,”anasema Mzinga ambaye anapanga biashara yake chini kandokando ya eneo hilo.

Sio wafanyabiashara tu, hata wakazi wa eneo hilo hawafurahishwi na vitendo hivyo na mmojawao ni Amina Mpembeja ambaye ana matumaini makubwa kwamba tatizo hilo litamalizika baada ya ujenzi huo kukamilika na milango kufungwa katika vituo hivyo.

“Tatizo hili linatukera kwa sababu watoto wetu wanaona yanayotendeka hapa. Tuhofia wanaweza kuiga,” anasema.

Hali halisi

Mwananchi Digital iliweka kambi katika eneo hilo kwa wiki mbili mfululizo na kubaini biashara ya ngono ikifanyika katika kituo hiko ambacho bado hakijaisha huku dada poa wakijiuza kwa bei tofauti kulingana na makubaliano na mteja.

“Ukitaka tufanye hapa (anaonyesha maboksi yaliyowekwa chini ndani ya kituo hicho) unatoa Sh3,000 kwa raundi moja na ukitaka gesti Sh5,000,” Grace anamwambia mwandishi.

Aidha, katika eneo hilo lililo katikati ya barabara pembezoni kuna vichochoro ambavyo vina ‘gesti bubu’ ambazo wateja watakaolipa Sh5,000 hupelekwa huko.

Kituo hicho cha mabasi yaendayo kwa haraka cha Mbagala Rangi Tatu ni miongoni mwa miradi ambayo inatekelezwa na Dart katika awamu ya pili kutoka Gerezani.

Jumla ya Sh253 bilioni zitatumika kukamilisha mradi huo ifikapo Oktoba, 2023.

Kama alivyobainisha Amina, huenda kukamilika kwa vituo hivi kunaweza kutatua tatizo hilo lakini hilo litategemea kwani wahenga walisema ‘tabia hujenga mazoea’.