Ripoti: Wakimbizi Afrika wazalisha Sh70 bilioni kwa mwaka
Pichani kutoka kushoto kwenda kulia ni Tito Mbathi, Msimamizi wa Kimkakati wa Ushirikiano katika Amahoro Coalition; Mable Ndahula, Mkurugenzi Mtendaji wa DFCU Foundation; na Maryann Wanjiku Michuki, Ofisa Mkuu wa Suluhisho za Biashara wa dfcu Bank, wakijadili fursa za uwekezaji kwa sekta binafsi katika jamii za wakimbizi wakati wa uzinduzi wa ripoti yenye kichwa “Hiding in Plain Sight: Africa’s $27 Billion Displacement Market Opportunity” uliofanyika Hoteli ya Serena Hotel Kampala hivi karibuni.
Muktasari:
- Ripoti inaonesha kuwa watu milioni 43.1 waliolazimika kuhama makazi yao barani Afrika wakiwamo wakimbizi huzalisha mapato yanayokadiriwa kufikia Dola 27 bilioni za Marekani (Sh70.8 trilioni) kwa mwaka
Dar es Salaam. Wakati wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makazi yao wakionekana kama wahitaji wa misaada ya kibinadamu, ripoti mpya imebaini kundi hilo lina nguvu kubwa ya kiuchumi inayoweza kuchochea ukuaji wa Afrika lakini bado halijapewa fursa na huduma zinazostahili.
Hayo yamebainishwa kupitia Ripoti ya ‘Hiding in Plain Sight: Africa’s $27B Displacement Market Opportunity’ iliyozinduliwa hivi karibuni na Amahoro Coalition.
Ripoti hiyo inaonesha watu milioni 43.1 waliolazimika kuhama makazi yao barani Afrika wakiwamo wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi zao (IDPs) huzalisha mapato yanayokadiriwa kufikia Dola 27 bilioni za Marekani (Sh70.8 trilioni) kwa mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, fedha hizo ni sawa na Pato la Taifa la Uganda katika miaka ya 2010 au Zambia ya sasa.
Hata hivyo, uchumi huo unaendesha shughuli zake bila miundombinu ya kifedha ambayo kawaida hupatikana katika uchumi wa ukubwa huo, ikiwamo huduma za benki, minyororo rasmi ya biashara za rejareja na upatikanaji wa mikopo.
Mkuu wa Ushirikiano wa Amahoro Coalition, Tito Mbathi amesema mtazamo wa kuwaona wakimbizi kama wapokeaji wa misaada pekee umeficha mchango wao mkubwa katika uchumi wa Afrika.
Amesema maelfu ya wakimbizi barani Afrika wanaendesha biashara ndogo na za kati, wanajihusisha na shughuli za kilimo biashara za kuvuka mipaka na huduma mbalimbali, lakini hukabiliwa na ukosefu wa mikopo, huduma za benki, masoko rasmi na mitaji ya kukuza shughuli zao.
“Jamii za wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makazi yao hazisubiri msaada. Wanaendesha biashara, wanalima na kushiriki katika biashara za kuvuka mipaka, lakini bila miundombinu ya kifedha inayopatikana kwa watu wengine. Hapo ndipo kuna fursa kubwa ya uwekezaji,” amesema.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sekta binafsi inaweza kunufaika kwa kuwekeza katika maeneo matano yenye uwezo mkubwa wa ukuaji ndani ya jamii hizo ambayo ni ujasiriamali, kilimo, huduma za kifedha, usafirishaji na ugavi wa bidhaa pamoja na viwanda vya uzalishaji.
“Changamoto kubwa si ukosefu wa shughuli za kiuchumi miongoni mwa wakimbizi, bali ni ukosefu wa mifumo inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi,” amesema.
Kwa kutambua fursa hiyo, Amahoro Coalition kwa kushirikiana na Benki ya DFCU ya Uganda, wameanza kubuni bidhaa maalumu za kifedha na programu za uwezeshaji wa biashara kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi nchini humo.
Ofisa Mkuu wa Suluhisho za Biashara na Masoko wa DFCU, Maryann Wanjiku Michuki amesema uzoefu wa taasisi hiyo unaonesha kuwa wakimbizi ni sehemu muhimu ya uchumi na wana uwezo wa kuwa injini ya ukuaji wa biashara endapo watapatiwa mazingira rafiki.
“Wakimbizi si wapokeaji wa misaada pekee. Ni wajasiriamali, wakulima, wateja na washirika wa maendeleo. Wanahitaji fursa za kupata mikopo, masoko na huduma za kifedha ili waweze kukuza biashara zao na kuchangia zaidi katika uchumi,” amesema.
Amesema ili kufanikisha hilo la kuwekeza katika jamii za wakimbizi, hakupaswi kuonekana kama jukumu la kibinadamu pekee, bali kama fursa ya biashara na maendeleo inayoweza kuleta manufaa kwa wawekezaji, Serikali na jamii zinazowahifadhi.