RITA: Idadi ya watoto waliopata vyeti vya kuzaliwa yazidi kupaa

Thursday June 16 2022
ritaapiic

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo akihutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa umri chini ya miaka mitano mkoani Tabora

By Maliki Muunguja

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wamebuni na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Usajili na Kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano hapa nchini kwa lengo la kuongeza kiwango cha usajili wa watoto ambao kama wananchi wengine wanahitaji nyaraka hiyo kwa matumizi mbalimbali.

Cheti cha kuzaliwa ni nyaraka ya awali na ya msingi kwani hutumika kama uthibitisho wa taarifa mbalimbali za mwananchi kama vile jina lake, umri wake, mahali alipozaliwa, taarifa za wazazi na nyinginezo.

Kwa hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la mahitaji na matumizi ya cheti cha kuzaliwa mara baada ya kuwepo kwa msukumo kwa taasisi nyingi za Serikali na binafsi kukitumia kuthibitisha taarifa hasa umri wa mtu. Mpango wa Usajili wa Wato-to unatekelezwa kwa kutoa huduma bila malipo karibu na makazi ya wananchi hii inamaana kwamba ugatuaji wa madaraka kutoka Serikali Kuu hadi serikali za mitaa umewezesha usajili kufanyika katika Ofisi za Watendaji Kata na Vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto.

Akizindua utekelezaji wa Mpango huu mkoani Tabora hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo aliyemwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kuwasajili watoto wao ili wapate vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo kupitia Mpango wa Usajili na Kuwapatia Vyeti vya Kuzaliwa hivyo kupata haki yao ya msingi ya kutambuliwa.

Ameongeza kuwa tangu kuzinduliwa kwa mpango huo hapa nchini mwezi Juni, 2015 idadi ya usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 umepanda kutoka 13% kwa takwimu za sen-sa ya mwaka 2012 hadi kufikia 65% kwa takwimu za mwaka 2021 hivyo ameipongeza RITA na wadau wote waliowezesha kupatikana kwa mafanikio hayo.

Mpaka sasa Mpango huu unatekelezwa katika Mikoa 22 ya Tanzania Bara na zaidi ya watoto 7,549,878 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bila malipo. Mkoa wa Tabora unakuwa Mkoa wa 23 kuanza kutekeleza mpango huu hapa nchini.

Advertisement

"Ni vyema viongozi katika ngazi zote wakafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango huu ili kuhakikisha watoto wanaosajiliwa ni wale walio na sifa stahiki na tuhakikishe wazazi wa watoto wanatambuliwa ipasavyo,’’ alisema Makondo.

Pia Alisisitiza kwamba ni vyema wazazi watambuliwe ipasavyo kwani Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa iliyo na muingiliano mkubwa wa raia kutoka nchi jirani na kwamba Serikali ilishatoa maelekezo kwamba vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka nyingine za utambuzi zishirikishwe kikamilifu katika zoezi hili na vitambulisho vya Taifa vitumike katika utambuzi wa wazazi wa mtoto atakayesajiliwa na kupatiwa cheti cha kuzaliwa.

Makondo aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huu.

"Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati Shirika la Umoja wa Mataifa linalohu-dumia watoto - UNICEF, Serikali ya Canada na Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu,’’ alisema Makondo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani aliyewakilish-wa na Katibu Tawala wa Mkoa, Msalika Makungu alisema kuwa Mkoa wa Tabora una Wilaya 7 na Halmashauri 8 ambazo zitatekeleza mpango huo kwa kutumia vituo vya Tiba na Ofisi za Watendaji Kata ambavyo jumla yake ni 542 na kutarajia kusajili watoto zaidi ya 549,167 walio na umri chini ya miaka mitano.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 9 tu ya watoto katika Mkoa wa Tabora wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hivyo idadi hiyo kuonesha wazi kuwa watoto wengi hawajasajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa na hivyo kushindwa kupata takwimu ili kuweza kupanga mipango sahihi ya huduma za afya na elimu.

"Maandalizi yote ya Msingi yamekamilika na naamini vituo vyote tayari vimeanza kutoa huduma. Kama sehemu ya maandalizi, tulifanya semina ya viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa, Wilaya na Halmashauri ambapo RITA walitupa elimu ya kina kuhusu mpango huu.

Kwa ujumla tumeuelewa, tumeupokea na tutausimamia kikamilifu na nakuhakikishia kwamba malengo yalitowekwa yatafikiwa ambapo tulikubaliana ni watoto wote walio na sifa za kusajiliwa wapate huduma hiyo,’’ Aliongeza Dkt. Batilda Buriani.

Naye Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory alisema mpango huo umesogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi na huduma kupatikana bure katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto na kwenye ofisi za Watendaji Kata.

Anatory aliongeza kuwa mpango huu umeweza kuimarisha mfumo wa kusajili, kutuma na kuhifadhi taarifa za waliosajiliwa kwa kutumia simu ya kiganjani (simu janja) iliyowe-kwa programu maalum ambapo taarifa hizo hutumwa moja kwa moja hadi kwenye kanzidata ya RITA Makao Makuu tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo nyaraka za taarifa za waliosajiliwa kusafirishwa kwa gari hadi Jijini Dar es salaam kutoka kila Wilaya kote Tanzania Bara.

"Kila kituo cha tiba kinachotoa huduma ya mama na mtoto na ofisi za watendaji wa kata wamekabidhiwa simu na vitendea kazi mbalimbali hivyo naamini kuanzia sasa taarifa za watoto wanaosajiliwa tutaziona moja kwa moja kupi-tia mtandao na tutaona nani anasajili na nani hafanyi kazi hiyo,’’ alisema Anatory.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwakilishi Mkazi wa Shirikia la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, Shalini Bahuguna alisema UNICEF imefanya kazi kwa karibu na Serikali kuanzia hatua za awali za Mpango wa Usajili wa Watoto na kuongeza kwamba ni haki ya Mtoto kutambuliwa hivyo kuipongeza Serikali ya Tanza-nia kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuhakikisha kwamba haki hii inapatikana kwa kila mtoto.

Aidha, aliishauri Serikali kuanza kutenga fedha katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri ili kuhakikisha Mpango wa Usajili unakuwa endelevu.

Naye Mkurugenzi Mwandamizi kutoka Ubalozi wa CANADA nchini, Helen Fytche alisema nchi ya Canada imeweza kuchangia zaidi ya Sh55 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Usajili wa Watoto ambao unaondoa vikwazo ili kuwawezesha watoto wote wa mijini na vijijini, maskini na matajiri na wasichana na wavulana kuweza kupata vyeti vya kuzaliwa.

 Aliongeza kwamba Mpango huu kielelezo cha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi ambao wameungana pamoja kuanzia hatua ya Ubunifu mpaka utekelezaji wa Mpango huu ambao umewezesha kusajili zaidi ya watoto 7.5milioni kuanzia mwaka 2013.

Kwa upande wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Innocent Rwetabura alieleza kwamba TIGO imeendelea kushiriki katika utekelezaji wa mpango huu tangu ulipoanzishwa kwa kutoa simu janja katika mikoa yote 23 ambazo hutumiwa na Wasajili Wasaidizi kutuma taarifa za watoto waliosajiliwa kwenda kwenye kanzidata ya RITA.

Kwa upande wa Moa wa Tabora zaidi ya simu 542 zimetolewa zenye thamani ya Sh46 Milioni.

Advertisement