Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rostam mmiliki mpya wa ndege za Coastal

Muktasari:

  • Ushindani katika sekta ya usafiri wa anga unatarajiwa kuongezeka nchini baada ya mfanyabiashara Rostam Aziz kuingia kwenye sekta hiyo akiwa na lengo la kufanya makubwa.


Dar es Salaam. Ushindani katika sekta ya usafiri wa anga unatarajiwa kuongezeka nchini baada ya mfanyabiashara Rostam Aziz kuingia kwenye sekta hiyo akiwa na lengo la kufanya makubwa.

Mwananchi imebaini kuwa, kupitia kampuni ya Taifa Aviation, mfanyabiashara huyo amenunua asilimia 51 ya hisa za Coastal Travels Company Limited kutoka kwa mwekezaji wa Kiitaliano mwenye asili ya Marekani, Carolina Colangelo.

Ununuzi huo wa hisa umemfanya Rostam kuwa mwekezaji mkuu wa shirika hilo la ndege kuanzia Septemba mosi, 2022.

Hata hivyo, kuna tetesi mfanyabiashara huyo anatarajia kununua asilimia 49 ya hisa zilizobaki, ili amiliki kampuni hiyo kwa ujumla wake.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Aziz ambaye ni mwekezaji mkubwa nchini katika sekta mbalimbali alisema: “Niko nje ya nchi, tukutane kwa mahojiano kuhusu hili nitakaporejea”.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Coastal Travels yenye historia ya zaidi ya miaka 30, ilishika nafasi ya nne mwaka 2021.

Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ndilo linaloongoza soko hilo kwa asilimia 52.9, ikifuatiwa na Precision Air na Auric Air zenye asilimia 22.8 na 10.3 mtawalia.

As Salaam Air ina asilimia 2.8 na mashirika mengine ya ndege yaligawana asilimia 8.6 ya hisa za soko hilo.

Katika jitihada za kuimarisha nafasi yake katika soko, Coastal Travels Ltd inapanga kununua ndege nyingine zaidi, zikiwemo kubwa.

Sasa hivi Coastal Travels inamiliki ndege 14, kati ya hizo 10 ni aina ya Cessna Grand Caravan C208B na nne ni Pilatus PC-12/45. Kwa sasa shirika hilo la ndege linafanya kazi katika maeneo zaidi ya 40.

Alipopigiwa simu ili kutoa maoni yake, Mkurugenzi mtendaji wa Coastal Travels, Kapteni Maynard Mkumbwa alisema menejimenti na mwekezaji mpya kwa sasa wanajadili hali ya kifedha ya shirika hilo.

“Hatujaanza kuzungumzia uwekezaji mpya na upanuzi chini ya mwekezaji mpya, lakini tunatarajia kufanya makubwa. Tunataka kuongoza soko katika sekta ya anga,” alisema. Kwa mwaka, shirika hilo lina wastani wa abiria 120,000, ikilinganishwa na 200,000 kabla ya Uviko-19.

“Chini ya mwekezaji mpya, pamoja na kudumisha usalama kama kipaumbele chetu cha kwanza, tutafanya huduma zetu kuwa bora zaidi,” alisema Kapteni Mkumbwa.

Mtaalamu wa masuala ya usafiri wa anga mwenye uzoefu wa miaka 34, John Chambo alisema, “uamuzi wake ni wa kupongezwa. Hata hivyo, ili afanikiwe, anahitaji kuwa na timu inayojua la kufanya.” “Tofauti na sekta nyingine, usafiri wa anga ni mgumu sana. Hii inaashiria kwamba fedha pekee hazitoshi, lazima afuate sheria za tasnia, ikiwa anataka kuifanya Coastal Travels kuwa imara,” alisema Chambo, mkurugenzi wa zamani wa huduma za urambazaji wa TCAA.

Mtaalamu wa masuala ya usafiri wa anga mwenye uzoefu wa miaka 47, John Njawa alimkaribisha bilionea huyo kwa tahadhari.

“Ataifanya Coastal (Safari) kuwa hai ikiwa atafanya uwekezaji mkubwa,” alisema.