Ruangwa washauriwa kulinda afya ya macho

Mratibu wa macho, Kasian Lukanga  akimpima macho Mkuu wa Wilaya Ruangwa, Hassani Ngoma katika uzinduzi wa zoezi la upimaji  macho  lililoendeshwa  na Taasisi ya Alata Charitable Foundation. Picha na Mwanja Ibadi.

Muktasari:

  • Taasisi imewafikia watu zaidi ya watu 500 ambapo 100 kati yao, watapatiwa miwani na wengine watapewa dawa na ushauri

Ruangwa. Katika juhudi za kuunga mkono Serikali ya awamu sita kwenye kutoa huduma za afya nchini, asasi ya kidini ya Alata Charitable Foundation wamefanya uchunguzi wa awali wa macho, kugawa miwani na matibabu kwa wananchi zaidi ya 500 wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa uchunguzi huo, Mratibu wa taasisi hiyo Rajabu Abubakari, amesema taasisi yake imeona umuhimu wa kuisaidia Serikali ya awamu ya sita kwenye kutoa huduma za afya ya kupima macho na matibabu ya awali.

Amesema Taasisi imewafikia watu zaidi ya watu 500 ambapo 100 kati yao, watapatiwa miwani na wengine watapewa dawa na ushauri

Rajabu   amewasisitiza wananchi kuacha tabia ya kutumia televisheni muda mrefu pamoja na vifaa vingine ambavyo vina miozi mingi ambayo inaweza kuathiri macho

“Fanyeni uchunguzi wa macho mara kwa mara ili kuweza kujua afya zenu,” amesema Abubakari.

Naye mratibu wa macho wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Kassian Lukanga, amesema changamoto ya macho imekuwa kubwa hasa kwa watu wenye umri kuanzia miaka 50 hivyo ni vyema wakachukua tahadhari ili kuyalinda macho yao.

Lukanga ameongeza kuwa pamoja na tatizo la macho; Wilaya ya Ruangwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya vituo vya kutolea huduma ya macho, kwani kati ya vituo 42 vya afya vilivyopo wilayani humo, ni vituo 2 pekee, ndivyo vinavyotoa huduma ya macho.

Mratibu huyo wa macho amesema watu wenye matatizo ya kuwashwa macho, presha ya macho pamoja na mtoto wa jicho; kupitia asasi hiyo, wananchi hao watapatiwa huduma za matibabu hayo bure.

Amina Juma mkazi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi amesema yeye alikuwa anaona macho yake yanawasha na kusababisha kutoa machozi ameishukuru taasisi ya hiyo kumsaidia kupata matibabu na atafuata ushauri aliopewa na matabibu ili hali isijirudie tena.

Awali Mkuu wa wilaya  ya Ruangwa Hasani Ngoma, amemtaka  mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa  pamoja na mganga mkuu wa wilaya kutoa taarifa kwa wananchi ili kujitokeza kwa wingi  wakati wadau wanapokuja kutoa huduma mbalimbali za afya.